Habari

Bajeti elimu bila malipo yapanda 15%

ELIMU bila ada kwa shule za msingi na sekondari imeongezewa bajeti yake kwa asilimia 15.34 kwa mwaka wa fedha ujao ikilinganishwa na bajeti iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Hayo yamo kwenye makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 yaliyowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki.

Kairuki ameliomba Bunge liidhinishe Sh bilioni 399.64 kwa mwaka 2023/2024 kwa ajili ya elimu bila ada ambazo kati yake, Sh bilioni 157.79 zimetengwa kwa shule za msingi na Sh bilioni 241.85 kwa sekondari.

“Bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la shilingi bilioni 53.15 sawa na asilimia 15.34 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi bilioni 346.49 iliyoidhinishwa katika mwaka wa Fedha wa 2022/23,” alisema Kairuki.

Alisema ongezeko hilo linatokana na wanafunzi wa kidato cha tano na sita kujumuishwa katika Mpango wa Elimu Bila Ada. Katika hatua nyingine, Kairuki amesema serikali itaendelea na mpango wa ujenzi wa matundu ya vyoo katika vituo shikizi ambako Sh bilioni 5.74 zimetengwa kwa ujenzi wa matundu 5,218 ya vyoo.

Aidha, zimetengwa Sh bilioni 5.52 kujenga matundu 5,020 ya vyoo kwa kidato cha tano na sita. Ujenzi wa mabweni 61 ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu umetengewa Sh bilioni 7.86. Zimetengwa pia Sh bilioni 2.58 kuendelea na ujenzi wa uzio wa mabweni ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Vilevile ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kidato cha tano na sita kwa shule za sekondari umetengewa Sh bilioni 47.89. Aidha, Kairuki alisema serikali itaendelea na mpango wa ukarabati wa shule kongwe za msingi na sekondari ambako Sh bilioni 37.49 zimetengwa. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 33.12 ni kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe 184 za msingi na Sh bilioni 4.37 ni za ukarabati wa shule kongwe za sekondari.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button