Habari

Bil 2.34/- za China kuendeleza utalii Hifadhi ya Kilimanjaro

SERIKALI ya China na Tanzania zimetiliana saini mkataba wa Dola za Kimarekani milioni moja sawa na Sh bilioni 2.34 kusaidia shughuli za kuendeleza utalii kwenye Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

Mkataba huo umesainiwa juzi kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro yaliyofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya hifadhi hiyo.

Wakati wa utiaji saini mkataba huo, Tanzania iliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Anderson Mutatembwa na Balozi wa China nchini, Cheng Mingjian.

Balozi Cheng alishukuru ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi yake na Tanzania. Alisema rais wao anaamini kuwa ili dunia ikae vizuri, ni lazima mazingira yaboreshwe.

Alisema fedha hizo zilizotolewa, msingi wake mkuu ni kusaidia kuhifadhi mazingira na kuweka vizuri miundombinu ya utalii kwa faida ya watalii na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa aliyeshuhudia tukio hilo, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua Tanzania duniani kupitia Mlima Kilimanjaro katika

filamu ya Royal Tour.

Alisema Mlima Kilimanjaro ni nembo ya Afrika kwani ndio mrefu kuliko yote barani humo na mkubwa duniani ambao upo huru kwa maana ya kwamba umesimama peke yake bila kuwapo kwa safu za milima kama ilivyo milima mingine duniani.

Alisema mlima umeendelea kuwa kivutio kikubwa cha watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, hivyo kutoa ajira kwa jamii iliyo jirani na taifa kwa ujumla.

Mchengerwa alitoa maelekezo kwa Shirika la Hifadhi la Taifa Tanzania (Tanapa) na wizara yake kuendelea kuboresha miundombinu na usalama kwa wageni.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button