
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametua mkoani Iringa kwa kishindo huku akiwatoa hofu watanzania kuhusu katiba mpya akisema chama hicho kimeshampa ridhaa na dhamana mwenyekiti wao, Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuanzisha mchakato huo.
Chongolo ametoa hakikisho hilo wakati akizungumza na wafuasi, viongozi na wanachama wa chama hicho waliompokea kwa bashasha hii leo mjini Mafinga anakotarajia kuanzia ziara yake itakayochukua siku sita mkoani Iringa kuanzia kesho.
“Tumesikiasikia huko watu wanazungumza wanataka katiba mpya. Waambieni CCM inataka katiba bora, itakayotupeleka namna gani, iweje na iandikwaje,” alisema chongolo.
Alisema wakati CCM inajadili namna kuendeleza mchakato huo ulisimama kwa miaka tisa bado kuna wachache wanaotaka jambo hilo lionekane kama lao wakijiita sisi ni sisi.
Katika mchakato huo, Chongolo alisema CCM inayo dhamira ya dhati na ya kweli itakayohakikisha Tanzania inapata Katiba mpya na bora.
Amewataka watanzania kuachana na wanasiasa wanaotoa ahadi hewa akisema katika mchakato wowote wa maendeleo hakuna miujiza kwa watu wasiofanya kazi.
Alisema chama hicho sio cha kurukaruka hewani kama nyani au ngedere kwani kina uzoefu wa uongozi na kinatambua mahitaji ya wananchi wake.
“Mimi na timu yangu tumekuja Iringa kukagua utekelezaji wa Ilani yetu kwasababu tuliahidi na tunajua watanzania wanataka maji, umeme, elimu, huduma za afya, barabara na huduma zote za kijamii,” aliongeza Chongolo.
Katika ziara yake mjini Mafinga kesho Chongolo atazindua mradi wa vibanda vya CCM, nyumba ya Katibu wa CCM, kushiriki ujenzi wa maji miji 28, kituo cha Afya Ifingo na kugawa vyandarua na baadaye kufanya mkutano wa hadhara.