Habari

DART yatoa msaada wa Sh milioni 8 hospitali rangi tatu

MENEJIMENTI ya Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) umetoa misaada wa Baiskeli moja ‘Wheelchair’, mashine ya kupimia mapigo ya moyo (BP), mashuka (40) sabuni dawa za mswaki na vitu vingine wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 8 katika Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu.

Msaada huo umetolewa kama sehemu ya kuadhimisha ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa jana Machi 8, 2023.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Wanawake wanaofanya kazi DART, Mwamvua Stambuli, amesema msaada huo ni sehemu ya upendo wa DART kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika Hospitali hiyo.

Amesema DART imeichagua Hospitali hiyo kwa kuwa hivi karibuni itaanza kutoa huduma za usafiri kwenda Mbagala hivyo hatua hiyo ni kama kuongeza upendo kwa wananchi hususani wagonjwa na uongozi wa hospitali hiyo.

“Hivi karibuni DART itaanza kutoa huduma ya usafiri kuja eneo hili la Mbagala, hivyo nasi kama wakina mama tumeona vyema kusambaza upendo kwa kuja na kuwafariji wanawake wenzetu waliolazwa mahali hapa ili kuwaonyesha ni namna gani tunawapenda” amesema Mwamvua

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dk Ali Makoli Musa, aliishukuru Menejimenti ya DART kwa msaada huo na kuonyesha kwao kuwajali wagonjwa waliolazwa mahali hapo huku akiwaomba watanzania wengine kuiga mfano huo kwa kuwa ni tukio la kijamii.

Amesema Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu inatoa huduma kwa wagonjwa wasiopungua 1200 kwa siku na kuwahudumia wanawake wanaojifungua 40 kwa siku, huku wodi ya wakinamama ikihudumia wazazi 60 kwa siku na kusisitiza kuwa ni Dhahiri kuwa inahitaji msaada wa vitu mbalimbali ili kutosheleza mahitaji ya wagonjwa hao wanaofika kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.

Aidha amesema changamoto iliyopo mahali hapo ni ufinyu wa eneo ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa inaowatibu kwa siku ambapo pia ameishukuru Serikali ya kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa litakalosaidia kukabiliana na tatizo hilo.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button