
SHIRIKA la HakiElimu Tanzania limesema kuwa licha ya serikali kuboresha sekta ya elimu, lakini bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ikiwemo mlundikano wa wanafunzi darasani.
Mkurugenzi wa HakiElimu Dk John Kalage amesema, kwa mujibu wa kitabu cha takwimu za elimu Tanzania (BEST) 2021 kinaonyesha uwiano wa darasa shule za msingi ni 1:74 badala ya 1:45 huku yale madarasa ya awali ukiwa ni 1:75 badala ya 1:40 unaotakiwa.
“Hii inafanya shule za msingi kuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa 102,485 ripoti ya CAG inaonyesha halmashauri 45 zina upungufu wa madawati 158,066 matundu ya vyoo 56,530, vyumba vya walimu 35,664 na upungufu wa madarasa 27,316.” Amesema
Amesema, pia changamoto nyingine ni uhaba wa walimu 100, 958 kwa shule za msingi sawa na asilimia 37 huku shule za sekondari uhaba wa walimu 74,743 sawa na asilimia 47.
“Pamoja na Tamisemi kupewa kibali cha kuajiri walimu 13,130 bado uhaba wa walimu itabaki kuwa walimu 162,571.” Amesema
Aidha, amesema kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia juu ya viashiria vya utoaji huduma katika mnyororo wa matokeo ya elimu (WB SDI Report, 2016) Idadi kubwa ya walimu bado hawana stadi za kitaaluma na uelimishaji zinazohitajika ili kufundisha ipasavyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uwezo wa maarifa miongoni mwa walimu wa kitanzania ulikuwa duni, ni mwalimu 1 tu kati ya walimu 5 aliyepata alama zaidi ya 80 katika jaribio lililojumuisha Kingereza na Hesabu.
Amesema kwa ujumla ni asilimia 59 tu ya walimu walikuwa na maarifa yanayostahili, kwa kutambua umuhimu wa mwalimu kuwa na umahiri unaoendana na wakati kitaaluma, serikali inaweka mkazo katika mafunzo endelevu ya wlaimu kazini (MEWAKA).
“Changamoto kubwa katika azma na mipango hii ni kukosekana kwa bajeti toshelezi ya utoaji mafunzo stahiki kwa walaaimu walioko kazini, mathalani mwaka wa fedha 2020/21 serikali iliwezesha mafunzo kwa walimu wa juu ya utoaji wa ushauri na unasihi kutoka shule 174 kati ya 3,863 za sekondari saw ana asilimia 4.5.
Aidha, amesema kwa mwaka 2021/22 serikali ilitoa mafunzo ya utekelezaji wa mtaala wenye kuzingatia umahiri kwa walimu 2,300 kati ya walimu 170,569 wa msingi saw ana asilimia 1.35 tu na walimu 1,941 kati ya 84,614 sawa na asilimia 2.3 wa sekondari.