
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amesema wizara yake kupitia Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) itaendelea kushirikiana na wizara za kisekta za uzalishaji katika kukuza uchumi, ujuzi na kuongeza ajira kwa vijana.
Bashungwa ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya uzalishaji mali katika shamba la mpunga na SumaJKT Mngeta Plantation na Kikosi cha Chita JKT yaliyopo mkoani Morogoro.
Alisema kwa sasa kumekuwapo na ushirikiano katika ya Wizara kupitia JKT na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya uzalishaji mbegu za mpunga na mahindi.
“Ushirikiano ambao upo na Wizara ya Kilimo ni maelekezo ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa tuwe wabunifu na kwa upande wa wizara tunalo jukumu kubwa sana la kuwa wabunifu kwa kushirikiana na wizara za sekta hususani sekta ambazo zinafanya uzalishaji.”Amesema Bashungwa
Alisema kuna vijana ambao wanajiandikisha kujiunga na JKT kwa mujibu wa sheria na kuna wale wanaojiunga kwa kujitolea kutokana na uzalendo wao wa kutaka kuwa sehemu ya mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa ili wapate ujuzi lakini wafundishwe uzalendo.
Kwa hiyo tunaposhirikiana na wizara za kisekta ambazo zinazalisha si tu kuwa tunatekeleza kile mheshimiwa Rais ametuagiza lakini ndio utekelezaji wa Ilani ya chama ya kuzalisha ajira milioni nane ambazo zinaweza kuzalishwa kwa wizara kushirikiana.”Amesema na kuongeza
“Na mimi niwashukuru waheshimiwa mawaziri wenzangu kwa ushurikiano, mmeona tulisaini hati ya makubaliano wizara ya kilimo na moja ya miradi iliyoko kwenye makubaliano hayo ni mradi huu wa Chita na SumaJKT Mngeta Plantation mmeona mafanikio hayo, hivyo kadili miradi hii inavyozidi kupanuka na kufanikiwa maana yake hata vijana wananufaika zaidi.” Amesisitiza
Alisema kwa sasa Wizara kupitia JKT iko kwenye mazungumzo na Wizara ya Mifugo na uvuvi sambamba na mpango wa uchumi wa blue kwa Zanzibar kupitia mradi wa ufugaji samaki ili kuibua fursa ambazo zitawanufaisha vijana katika sekta ya uvuvi.
Alisema uongozi wa JKT pia unaendelea na mazungumzo ya ushirikiano na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili vijana wa JKT ambao wamepata mafunzo stadi waweze kutumia kwenye taasisi za ufundi kama ya Uhandishi na Usanifu Mitambo Tanzania(TEMDO), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) na Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO).
Aidha, Bashungwa alisema Wizara yake kwa kupitia Jeshi la Kujenga Taifa itaendelea kuandaa majukwaa rasim ya kuelezea fursa ambazo jeshi hilo inazitengeneza ambazo zinaweza kusaidia wananchi.