Habari

Kamati hali ya hewa yakutana Arusha

TANZANIA imekuwa mwenyeji wa mkutano wa Kamati ya Kuchakata Data za Hali ya Hewa Duniani, lengo ikiwa ni kuhakikisha data za hali ya hewa zinatumika ipasavyo na taasisi za hali ya hewa katika nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kwa manufaa ya sekta mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Hamza Kabelwa amesema mkutano huo unashirikisha nchi 12 na kueleza kuwa una umuhimu mkubwa kwa nchi.

“Kwanza ni kutangaza utalii wa nchi yetu, ambapo wageni hawa watakuwa mabalozi wa vivutio vya Tanzania katika nchi zao, aidha, kutokana na changamoto kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, upatikanaji data sahihi za hali ya hewa ni muhimu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania katika kusaidia kukabiliana na mabadiliko hayo, ili kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk David Richardson, alisema Kamati anayoisimamia itajikita katika kusaidia kujenga uwezo na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wote, ili kulinda maisha ya watu na mali zao.

Mwenyekiti wa Kamati, Dk David Richardson

Kwa upande wake, Dk Anthony Rea, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu WMO alisema, majukumu ya kamati hiyo yanaenda sambamba na jitihada mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na WMO za kusaidia nchi kufanikisha upatikanaji wa data za uangazi za hali ya hewa, ambazo zinazaa taarifa za hali ya hewa kwa matumizi ya nchi wanachama wa WMO.

Nchi zinazoshiriki mkutano huo unaofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuanzia Machi 20 -24,  2023 ni Australia, Brazil, Canada, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Korea ya Kusini, Japan, Afrika Kusini, Hispania, Uingereza na Marekani.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button