Habari

Kampuni ya mbolea yaanza mikakati uboreshaji huduma

KAMPUNI ya Yara inayojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa mbolea bora za kupandia na kukuzia mazao, imeanza kuzalisha na kusambaza lishe bora ya mifugo kama sehemu ya mikakati yake ya kupanua wigo na kuongeza huduma mpya katika sekta ya kilimo na ufugaji nchini.

Uzinduzi wa bidhaa hizo mpya za lishe ya mifugo umefanywa leo mjini Iringa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakiwemo wawakilishi wa wafugaji kutoka wilaya zote za mkoa huo.

“Nawapongeza sana Yara kwa uamuzi huu ambao sio tu ni muhimu kwa wafugaji wote nchini lakini pia ni wenye faida kwa uchumi endelevu wa Taifa letu,” alisema.

Alisema bidhaa hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa kuchochea uzalishaji wa bidhaa za ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na hata samaki na kudhihirisha mchango wa wafugaji na wavuvi katika kuboresha maisha ya watanzania na kuchangia ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Akizungumzia hali ya sasa ya uzalishaji katika sekta hiyo, Dendego alisema; “Licha ya kwamba Tanzani ni ya tatu barani Afrika kwa wingi wa mifugo, uzalishaji wa maziwa, nyama na mayai bado ni wa kiwango duni na kusababisha pia mchango wake katika ukuaji wa uchumi kuwa mdogo kwa kiwango cha asilimia saba.”

“Kampuni ya Yara leo inafungua njia sahihi ya kuchangia katika juhudi za kuikwamua sekta ya ufugaji kwa kuleta sokoni lishe bora ya mifugo itakayoongeza kiwango cha uzalishaji wa nyama, maziwa, samaki na mayai kwa haraka,” alisema.

Awali Mkurugenzi wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo alisema wameanza kuzalisha na kusambaza bidhaa hiyo baada ya kubaini kuna upungufu wa lishe bora ya mifugo nchini katika kuongeza tija katika sekta hiyo.

“Tumezindua bidhaa saba ambazo zikitumiwa ipasavyo katika sekta hiyo ya mifugo zitachangia kwa kiwango kikubwa kuongeza tija na kuinua kipato cha mfugaji na uchumi wa Taifa,” alisema.

Akizungumzia uchumi mdogo kwa wafugaji wadogo wa Tanzania kumudu kununua bidhaa hizo, Odhiembo alisema; “bidhaa hizo zitafungwa katika ujazo utakaomuweza kila mfugaji kununua kulingana na uwezo na mahitaji yake.”

Akitoa mfano wa lishe hizo za mifugo aliizungumzia bidhaa ya Maziwa Pro aliyosema imelenga kuwasaidia wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuwaepusha na magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na upungufu wa madini.

Taarifa ya Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) inaonesha wakati mahitaji ya maziwa nchini ni wastani wa lita bilioni 12 kwa mwaka, kuna upungufu wa wastani wa lita bilioni tisa ambazo zimekuwa zikiigharimu nchi zaidi ya Sh Bilioni 23 kuagiza nje ya nchi.

Baadhi ya wafugaji wamepongeza ujio wa bidhaa hizo za lishe ya mifugo kwa matarajio makubwa kwamba utaongeza tija katika sekta hiyo.

Mmoja wa wafugaji hao, Denis Godwin wa Kilolo alisema; “Nitaanza kutumia bidhaa hizo mara moja nikiamini kwamba zina ubora unaozungumzwa na ni muarobaini katika kuiboresha sekta ya mifugo na kuongeza uzalishaji.Naamini kama zisingekuwa na ubora unaozungumzwa serikali isingekubali ziingizwe sokoni.”

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button