Habari

Madiwani wataka migogoro ya mipaka ishugulikiwe Mpanda

Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, limemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo kushughulikia suala la mipaka kwenye baadhi ya Kata kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na migongano.

Meya wa Manispaa ya Mpanda, Haidary Sumry ameyasema hayo katika kikao cha kuhitimisha robo ya pili ya utekelezaji wa maendeleo ya Kata baada ya Diwani wa Kata ya Kasokola, kuibua hoja ya tatizo la mipaka katika baadhi ya vijiji ndani ya kata hiyo.

“Tukuombe Mkurugenzi timu yetu ya watu wa ardhi ikienda huko iende ikafanye kazi ya kumaliza kazi, naona jambo hili linajirudia rudia sana hasa kwenye Kata ya Kasokola,” amesema Sumry na kuongeza kuwa.

“Kwanza kulikuwa na shida Kata ya Shanwe wakaenda wakamaliza, leo tunaambiwa kuna shida Kata ya Katumba, Kanoge na baadhi ya maeneo jirani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, kwa hiyo tukuombe Mkurugenzi ulichukulie kwa uzito,”  amesema.

Katika hatua nyingine baraza hilo limelaani kitendo cha watoto kuzagaa mitaani wakifanya shughuli za kuokota na kuuza vyuma chakavu kwa kile walichodai kitendo hicho kinaweza kuongeza wizi na udokozi mitaani.

Diwani wa Kata ya Majengo William Mbogo ameeleza kumekuwa na wimbi kubwa la watoto kuonekana katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Majengo, wakiwa wamebebelea vyuma chakavu ambavyo inasemekana vyuma hivyo huuzwa kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu.

“Majuzi umefanyika wizi wa miundombinu ya vyuma vya meza na viti vya chuma kwenye Shule za Msingi Azimio na Majengo,”amesema.

 

 

Mbogo ametoa wito kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu Manispaa ya Mpanda kutojihusisha na ununuzi wa chuma chochote cha mali ya umma kwani kufanya hivyo ni kuihujumu serikali.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Mpanda, Haidary Sumry akichangia hoja hiyo amesema kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf, ameshatoa maelekezo kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu kutofanya biashara hiyo na watoto.

“Mkuu wa Wilaya alishasema mfanyabiashara atakayekutwa akifanya biashara hiyo na watoto hatasita kumfutia leseni mfanyabiashara huyo,” Sumry ameliambia baraza hilo.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button