Habari

Mambo yaiva bweni la wasichana Shule ya Kabungu

Shule ya Sekondari Kabungu iliyopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi yenye kidato cha kwanza hadi sita iko mbioni kukamilisha  ujenzi wa bweni la wasichana lililogharimu kiasi cha Sh Milioni 150.

Akizungumza mara baada ya Mkuu wa wilaya ya Tanganyika kufika katika shule hiyo na kukagua maendeleo ya ujenzi wa bweni hilo,  Mkuu wa shule ya sekondari Kabungu, Abdallah Dawa amesema awali kutokana na kutkuwa na bweni wanafunzi walikuwa wakipanga mitaani, hivyo kuwa na changamoto nyingi katika malezi na baadhi kujikuta wakipata mimba.

Amesema mbali na tatizo la watoto hao kupata mimba za utotoni, pia wanafunzi wengi walikua wakitumia fursa hiyo kutoroka au kutofika kabisa shuleni.

“Tulikubaliana na wazazi kuwa watoto wote wapate chakula shuleni na wahame kutoka magetoni wahamie shuleni, nashukuru mungu tulifanikiwa kwa asilimia 100 baada ya kuwa na muitikio mkubwa na wanafunzi wote kuhamia hapa, tukajikuta tuna changamoto ya wanafunzi kulala darasani,” amesema na kuongeza:

“Hapo ndipo tulilazimika kuibua mpango maalumu wa kuhakikisha tunajenga bweni na wanafunzi wanaondoka kulala kwenye madarasa na kuingia mabwenini,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, amesema watahakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa bweni hilo na matarajio yao ifikapo Febuari 15 mwaka huu bweni hilo litaanza kutumika.

Amesema wameweka mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba, kaya kwa kaya, kitongoji kwa kitongoji ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyumbani pasipo kwenda shule.

“Tutapambana kutafuta fedha kama ambavyo Rais ameelekeza, wanafunzi waliopo hapa ni zaidi ya 1,670 tutahakikisha kuwa wote wanasoma hakuna atakayeacha masomo hata mmoja,”amesema Buswelu.

Maria Patrick ni miongoni mwa wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule hiyo, amesema kukamilika kwa bweni hilo kutasaidia ufalu kuongezeka kwa wanafunzi na kupunguza utoro mashuleni.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button