
MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Jokate Mwegelo amezindua mbio za mama mjamzito zijulikanazo kama ‘Mamathon’, ambazo zina lengo la kuitaka jamii kumpa ulinzi mjamzito na kuona anajifungua salama.
Ameyasema hayo Mei 25, 2023 kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ambapo amesema kuwa mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Mei 28, mwaka huu kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mazoezi.
“Lengo letu la kuanzisha Korogwe Mamathon ama Mwendo wa Mama, ni kuwahamasisha akina mama wanapopata ujauzito basi waone hilo ni jambo la fahari na wanatakiwa kujivunia sababu wanatuletea viumbe hapa duniani.
“Na kwa kutambua Mwendo wa Mama, na sisi tuna wajibu wa kumuenzi mwanamke kwa cheo kikubwa cha kuitwa Mama. Hivyo ni lazima mama huyu apate huduma muhimu zitakazomuwezesha kujifungua salama,” amesema Mwegelo.
Mwegelo amesema Rais Dk Samia Suluhusu Hassan ndiyo amempa msukumo wa kuanzisha jambo hilo la kuwasaidia wanawake wajawazito, kwani ameboresha huduma za afya kwa kujenga miundombinu ya vituo vya afya, zahanati na hospitali karibu nchi nzima, na hata Wilaya ya Korogwe ni wanufaika wa maboresho hayo kwenye sekta ya afya.
Mwegelo amesema kuwa mbio hizo zinatarajiwa kuwahusisha wanawake zaidi ya 1,700, ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wanatarajiwa wanawake 1,000, na Halmashauri ya Mji Korogwe wanawake 700.
“Wanawake wanaotaka kuhudhuria wakajiandikishe kwenye vituo vya afya. Tumeelezwa wanawake 700 watatoka Halmashauri ya Mji Korogwe, na 1,000 kutoka Halmashauri ya Wilaya. Kutakuwa na huduma mbalimbali za vipimo, ikiwemo virusi vya UKIMWI, shingo ya kizazi, presha, malaria, wingi wa damu, na vipimo vingine,” amesema Mwegelo.