Habari

Mtaalamu: TB inaweza kusababisha ugumba

WENGI wanafahamu kuhusu athari mbalimbali za kiafya za ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB), lakini pengine hawafahamu miongoni mwa athari hizo unaweza kusababisha ugumba kwa wanaume na wanawake.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma jijini Dar es Salaam, Dk Mbarouk Seif Khaleif ugumba huo unaweza kutokea kwa mwanaume endapo korodani imepata maambukizi ya TB huathirika uzalishaji mbegu za uzazi, wakati mwanamke kama amepata maambukizi huathirika mfuko wa uzazi, hali inayosababisha kushindwa kubeba mimba.

Amesema mwanaume mwenye TB katika koradani asipobainika mapema atakuwa akisumbuliwa na maambukizi katika mfumo wa mkojo mara kwa mara ‘UTI’, wakati mwanamke atakuwa akisumbuliwa na maambukizi kwenye via vya uzazi ‘PID’.

“Mtu asipogundulika mapema kila siku atakuwa anaumwa UTI na PID atamaliza dawa zote tatizo halitaisha, miaka na miaka inaenda mwanamke mimba hapati, mwanaume hawezi kuzalisha, kumbe ni TB katika mfumo wa uzazi,” amesema.

Dk Seif amesema kimila imezoeleka jukumu la kubeba ujauzito ni mwanamke, lakini kisayansi mama na baba wote wana uwezo sawa na asilimia 30 ya ugumba inaweza kuwa baba au mama, japo jamii nyingi inamsingizia mama.

“Sababu za wanaume kuwa wagumba huwa tunasema ili mwanaume awe na uwezo wa kumpa ujauzito mwanamke awe na idadi sahihi na mbegu sahihi, kwa sababu unaweza ukatoa mbegu na zikawa hazitembei au ni ndogo.

“Maambukizi ya ugonjwa wa TB kwenye korodani inaweza kusababisha mbegu zisiwe sahihi na hivyo mwanaume kushindwa kutungisha mimba,” amesema.

Aidha kwa upande wa wanawake kuwa na tatizo la ugumba ameeleza kuwa kwa wanawake mfumo mzima wa afya yake ya uzazi na hedhi unaanzia kichwani mwake kwenye ubongo, ambapo kuna homoni za ‘Pituitary na Hypothalamus’ ambazo zina-control hedhi na mayai ya mwanamke pamoja na msongo wa mawazo.

Hata hivyo, Dk Seif amesema kuwa TB inaweza kushambulia kiungo chochote cha mwili na kuitaka jamii kujenga utaratibu wa kupima mara kwa mara.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button