Habari

Mwalimu auawa na mpenzi, kisa milioni 13/- za mkopo

MWALIMU wa Shule ya Msingi Lagangabilili mkoani Simiyu, Monica Patrick anadaiwa kuuawa na mpenzi wake, Muddy Ramadhan ili apate Sh milioni 13 ambazo mwalimu huyo alikuwa amepata mkopo kutoka Benki ya NMB.

Kwa mujibu wa shemeji wa marehemu, Oscar Abinery aliyezungumza na HabariLEO jana, mtuhumiwa Ramadhani ni mganga wa jadi na inadaiwa alimuua Mionica kwa kumdidimiza kwenye magugu ya Ziwa Victoria mjini Musoma mkoani Mara.

Abinery alisema shemeji yake alikwenda Musoma ili kumtembelea mganga huyo ambaye alimpokea kwenye kituo cha basi na kwenda naye hadi ziwani kukamkarimu mpenzi wake kwa upepo wa ziwani.

Hata hivyo, Abinery anadai baada ya kufika mwaroni mwa Ziwa Victoria, alimpa soda ambayo ilikuwa imechanganywa na dawa aina ya Valium ambayo ilimlewesha na kisha kumdidimiza kwenye magugu kando kando ya ziwa hilo, na kusababisha kifo chake.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk Osmund Mganga, amethibitisha kuwa mwili wa Monica umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha hospitali hiyo.

Licha ya kutokuwa tayari kuzungumzi suala hilo kwa kina jana, Dk Mganga alisema: “Ninachoweza ni kukuthibitishia kuwa mwili huo upo na askari wanaelekea chumba cha maiti kuufanyia postmoterm (uchunguzi)”.

Baada ya simu ya Kamanda wa Mkoa wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Mara, Longnus Tibishubwamu kutopokewa  kwa muda mrefu, moja ya chanzo cha habari cha uhakika kilichopatikana ndani ya jeshi hilo mjini Musoma kilithibitisha makachero wa kituo cha kikuu mjini hapo walikuwa wakielekea kwenye hospitali hiyo kutekeleza jukumu hilo.

Moja kati ya namba za simu zilizo kwenye tangazo lililotolewa na Familia ya Mwalimu Herman Mlale wa Kilimanjaro Siha, Sanya Juu kwenye mitandao ya kijamii, ilipokewa na aliyejitambulisha kuwa dada wa Monica, Furaha Patrick alikiri kuwa mdogo wake huyo amefariki dunia.

“Tumepata taarifa kuwa Monica amefariki dunia, mimi nipo Kilimanjaro lakini baadhi ya ndugu wameshafika Musoma,” alisema kwa njia ya simu.

Awali tangazo hilo lililoeleza kuwa Monica alipotea katika mazingira ya kutatanisha, liliibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii ambapo kundi moja la WhatsApp mjadala uliashiria kuwamo watu waliopata taarifa kuhusu tukio hilo.

Ilielezwa kuwa mwili wa Monica ulibainika juzi ukiwa umedidimizwa kwenye magugu kandokando ya Ziwa Victoria, Musoma huku mshukiwa wa kwanza akiwa mganga huyo wa jadi ambaye walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

“Ni binti mwenye mtoto mmoja, kuna taarifa mwili wake umepatikana mkoani Mara na alikuwa kazikwa kabisa na kwa mujibu wa watu wake wa karibu inavyoonekana alikuwa na mahusiano mapya yaliyompelekea umauti,” ilielezwa.

Ilielezwa inasadikika mahali alikouliwa ni karibu na anakoishi mwanaume huyo ambaye baada ya kubanwa na askari polisi, alikiri kumuua kwa kumdidimiza kwenye magugu kando kando ziwa Victoria.

Inadaiwa nguo za marehemu zilisahaulika maeneo alikozikwa, watu wakawa wakijiuliza kuhusu nguo hizo na maeneo hayo.

Inadaiwa mtuhumiwa Alijaribu kurudi ili kuondoa nguo hizo na kuhamisha maiti, ndipo alikamatwa na polisi. Hadi jana, mwili wa marehemu ulikuwa chumba cha kuhifadhiwa maiti hospitalini Musoma na kwamba utapelekwa Itilima kuagwa kabla haujasafirishwa Kilimanjaro, kuzikwa.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button