
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaibu Kaim amewaonya wananchi kutofanya shughuli yoyote ikiwemo kilimo na ufungaji karibu na vyanzo vya maji kwani ni kinyume cha sheria na ni uharibifu wa mazingira.
Shaibu ameyasema hayo leo Mei 25, 2023 jijini Dar es Salaam akizindua mradi wa utunzaji mazingira kwenye visima vya maji wilaya ya Kigamboni vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (DAWASA).
Amesema, hairuhusiwi kwa mtu yeyote kufanya shughuli yoyote ya kibinadamu au maendeleo yoyote ndani ya mita 60 kwenye vyanzo vya maji.
Amesema kuwa hatua hii ni muhimu kwa ajili ya kulinda na kuviendeleza vyanzo vya maji pamoja na uoto wa asili ikizingatiwa kuwa maji ni uhai.
“Tuendelee kuunga mkono juhudi za Serikali za upandaji wa miti kwa kupanda miti rafiki yenye kutunza mazingira katika vyanzo vyetu vya maji,” amesisitiza Kaim.
Amesema Mwenge wa Uhuru Kitaifa umekagua taarifa na hatua mbalimbali za mradi na umeridhika na utekelezaji wake.
“Niwapongeze DAWASA kwa jitihada kubwa mnazozifanya za kulinda na kuendeleza mazingira kwa kutunza vyanzo vya maji, mnafanya kazi nzuri, niwapongeze sana.”Amesema
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Kiula Kingu amesema katika jitihada za kutunza na kuendelea vyanzo vya maji Kigamboni, Mamlaka imetekeleza mradi wa kupanda miti ya matunda na ya kivuli 3300 kwenye visima virefu 11 vilivyopo.
“Huu ni mpango endelevu ambapo katika awamu ya kwanza tumeanza kupanda miti 1,800 kwenye eneo la tenki kubwa la maji.” Amesema.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa zimeongozwa na kauli mbiu ‘Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa’