Biashara

Ndege ya mizigo yakamilika, kutua nchini karibuni

SERIKALI inajiandaa kupokea ndege ya mizigo kati ya ndege tano mpya zikiwemo za abiria.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), John Nzulule alilieleza HabariLEO jana kuwa wamewasiliana na kampuni ya Boeing ya Marekani ikawaeleza kuwa muda wowote kuanzia sasa ndege hiyo itakuwa tayari kukabidhiwa.

“Timu ya Tanzania ya mwisho kwenda kukagua itakuwa tayari wakati wowote kufanya hivyo na habari zaidi tutawajulisha,” alisema Nzulule.

Awali katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa kampuni hiyo jana waliweka picha ya ndege hiyo namba 767 5H-TCO ikionesha iko tayari baada ya kufanyiwa majaribio ya kuruka.

Februari mwaka huu, Nzulule alisema ndege hiyo itawasili nchini kati ya Machi au Aprili mwaka huu na ndege nyingine nne zinatarajiwa kuwasili nchini kwa nyakati tofauti mwaka huu.

Juni mwaka jana, katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23, alisema serikali imefanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mpya tano.

Dk Mwigulu alisema mkakati wa serikali ni kuendelea kutekeleza mpango wa kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na katika kipindi cha mwaka 2021/22 serikali ilipokea ndege tatu.

Aidha, malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mpya tano uliofanywa unahusu ununuzi wa Boeing 737-9 (2) ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400, ndege moja Boeing 787-8 Dreamliner na ndege moja ya mizigo aina ya Boeing 767-300F.

Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa serikali imedhamiria kuboresha sekta ya usafiri wa anga na imejipanga kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

“Tunanunua ndege nyingine mpya tano, ATCL wameshasaini mkataba na kampuni moja ya kutengeneza ndege, lengo letu tununue ndege kubwa ya masafa marefu moja na nyingine kubwa ya mizigo, tumepata soko hata la mazao na mbogamboga hivyo lazima tuwe na uhakika wa usafiri ili visiharibike,” alisema Msigwa.

 

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button