Habari

Polisi yachangiwa gari, pikipiki

DHANA ya ushirikishwaji jamii imeendelea kulifaa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa hii leo likipokea msaada wa gari moja aina ya Toyota Premio lenye thamani ya Sh milioni 19 na pikipiki moja aina ya Boxer yenye thamani ya Sh milioni 3.1.

Msaada huo unaolenga kuimarisha doria na kupambana na uhalifu umetolewa na kampuni ya Mufindi Wood Poles Plant and Timber Ltd ya wilayani Mufindi iliyotoa gari hiyo na kampuni ya Udzungwa Corridor ya wilayani Kilolo iliyotoa pikipiki.

Akizungumza na wanahabari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi alisema vitendea kazi hivyo vimepatikana kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Jeshi la Polisi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Pamoja na msaada huo alisema jeshi la Polisi limefanya matengenezo ya magari 12 yaliyofanyiwa ukarabati wa jumla na kupakwa rangi upya.

ACP Bukumbi alisema zaidi ya Sh milioni 28.6 zilizopatikana kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo kampuni ya Asas Group, Ivory na Toyota Tanzania Ltd zimetumika katika matengenezo hayo.

Alisema magari hayo yatatumika katika kuzuia na kupambana na uhalifu ikiwemo udhibiti wa doria za barabarani ili kuzuia ajali zinazosababishwa na madereva wasiotii sheria.

“Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa tunatoa shukrani za dhati kwa wadau wote waliojitolea na tunaomba wengine wenye moyo huo wajitokeze ili tuweze kuongeza ushirikiano na kuifanya jamii ya wananchi wa Iringa kuwa salama,” alisema.

Mwakilishi wa kampuni ya kampuni ya Mufindi Wood Poles Plant and Timber Ltd Awadh Nyagongo alisema kama wadau muhimu wa maendeleo wa mkoa wa Iringa wameguswa na juhudi za jeshi la Polisi katika kukabiliana uhalifu na kuamua kutoa msaada huo ili uwasaidie kuongeza ufanisi.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button