

Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema kundi la hujuma la Ukraine limeingia eneo la mpaka wa Urusi leo na kuwafyatulia risasi raia kadhaa na kuita “kitendo cha kigaidi”.
Hapo awali Gavana wa Mkoa wa Bryansk alisema “wahujumu kutoka Ukraine” walifyatua risasi gari la raia huko Lyubechane, kijiji cha mpakani na kuua mtu mmoja na kumjeruhi mtoto.
Mykhaylo Podolyak, mshauri wa Rais wa Ukrain Volodymyr Zelensky, alituma ujumbe kwenye Twitter kwamba ni “uchochezi wa kimakusudi”. “Urusi inataka kuwatisha watu wake ili kuhalalisha shambulio dhidi ya nchi nyingine,” alisema.
Hapo awali Urusi iliripoti mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani za Ukraine katika maeneo ya mpaka wa Urusi, pamoja na Mkoa wa Bryansk. Lakini hakujawa na ripoti zilizothibitishwa za vikosi vya ardhini vya Ukraine kupenya Urusi.