Habari

RC Mtwara: Waharibifu vyanzo vya maji wachukuliwe hatua

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abas amevitaka vyombo vinavyohusika na uchukuaji hatua katika suala la uharibifu wa vyanzo vya maji kutowafumbia macho watakaohusika na uharibifu au ukataji miti kwenye vyanzo hivyo.

Akizungumza leo mkoani Mtwara katika zoezi la upandaji miti rafiki wa maji, mkuu wa mkoa huyo amesema mtu yoyote anayetaka kukata mti ni lazima aombe kibali kwa mamlaka husika.

“Watu wanapokata tu miti bila kuomba vibali kuna uwezekano miti hiyo ikaisha halafu tukakosa utunzaji mzuri wa mazingira na athari kwa Wananchi kwahiyo haya niliyoyasisitiza yazingatiwe.”amesema Kanali Abas.

Mkurugenzi wa Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini, Jumanne Sudi amesema chanzo hicho kina jumla ya visima vinane vilivyochimbwa na kati ya hivyo sita vinatumika kwenye uzalishaji wa maji na vina uwezo wa kuzalisha kiasi cha lita za ujazo milioni 12 kwa siku .

Amesema katika eneo la chanzo hicho miti 1300 imepandwa ambapo kwa Mkoa wa Mtwara unatarajiwa kupandwa miti 70,000 kwenye halmashaauri za mkoa huo.

Mhifadhi wa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Peter Nguyeje amesema miti hiyo itasaidia katika utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa udongo, maji, matumizi ya ujenzi wa nyumba zao lakini pia chanzo kikubwa cha mapato kwa taifa na mwananchi mmoja mmoja.

“Kwahiyo miti hii isipopandwa vizuri na kuitunza inaleta athari ikiwemo kukosekana kwa mvua, vyanzo vya maji kukauka hali ambayo inatokana na uharibifu wa miti hii kwenye vyanzo vya Maji.

Zoezi hilo limefanyika Kimkoa kwenye chanzo cha Maji cha Mtawanya kilichopo Kata ya Mtawanya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara chini ya Bodi ya Maji Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button