
SH trilioni 6.1 zimetolewa mkopo na ruzuku kwa wajasilimali milioni 8.6 ambao wameimarisha shughuli zao za biashara na uwekezaji. Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa ameeleza.
Ben’gi amesema hayo katika maonyesho mifuko na program za uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayofanyika mjini Kigoma. Amesema kuwa mikopo hiyo imewezeshwa kupitia program na mifuko ya uwezeshaji 72 inayosimamiwa na baraza hilo tangu ilipoanza miaka 20 iliyopita.
Alisema kuwa hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, mifuko na program hizo za uwezeshaji zimewezesha kutolewa kwa mikopo hiyo kwa wajasiliamali hao ambao kati yao wajasiliamali wanawake wakiwa ni milioni 4.7 na wanaume milioni 3.9 ambapo ajira milioni 17.6 zimetengenezwa.
Katibu huyo mtendaji wa NEEC alisema kuwa serikali imejipambanua katika kutekelezaji mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi hivyo uwepo wa mifuko hiyo ni utekelezaji wa mpango huo na kwamba maonyesho hayo kufanyika Kigoma kunatekeleza azma ya serikali ya kuufanya mkoa huo kuwa wa kimkakati kiuchumi.
Akizungumza katika maonyesho hayo Afisa Habari na Mawasiliano wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Christina Njovu alisema kuwa ni jambo muhimu kwa wajasiliamali kusajili majina ya biashara zao na kampuni ziweze kutambulika ndani na nje ya nchi kwa urahisi.
Njovu alisema kuwa BRELA inasajili leseni kundi A ambazo kiasi kikubwa zinahusu wafanyabiashara wanaofanya biashara za kuvuka mpaka hivyo wajasiliamali na wafanyabiashara wa Mkoa Kigoma ambao wako mpakani itawapa nafasi nzuri ya kufanya biashara ya kuvuka mpaka na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Burundi.
Meneja huyo wa Brela alisema kuwa katika upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiliamali wanaovuka mpaka kusajili kampuni na majina ya biashara ni mambo muhimu na kwa sasa usajili huo unafanyika kupitia njia ya mtandao na wajasiliamali wanaweza kujisali mahali popote walipo.
Akifungua maonyesho hayo Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amesema kuwa maonyesho ya sita ya mifuko na program ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayofanyika mkoani humo yataongeza chachu kwa watu mbalimbali kupata habari na taarifa ambazo zitasaidia kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na uwekezaji.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Salum Kalli mkuu huyo wa mkoa kuwa mifuko hiyo ni muhimu kwa wazalishaji na wawekezaji kupata taarifa za fursa zinazopatikana kwenye mifuko hiyo ikiwemo mikopo na uwezeshaji.