
SHIRIKISHO la Vyuo Vikuu vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) limemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya elimu, ikiwa ni pamoja na kuwaongeza fedha ya kujikimu kutoka Sh 8,500 hadi 10,000 kwa siku.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa TAHLISO, Frank Nkinda Dar es Salaam jana, Kamishna wa Mikopo wa shirikisho hilo, Emmanuel Martin alisema Rais Samia ana nia njema na wanafunzi na vijana wa nchi hii ndiyo sababu anafanya juhudi kubwa kuboresha mazingira ya elimu.
“Tuliomba nyongeza ya fedha ya kujikimu kwa Rais(Samia), asingekuwa na nia njema na sisi wanafunzi asingeweka ongezeko hilo la fedha ya kujikimu,” alisema.
Aliongeza kuwa ni wajibu wao wanafunzi kwenda kutafsiri nia hiyo na maono ya Rais Samia na kuyafanyia kazi ili azma na nia yake itekelezeke.
Alisema wako watu wanaobeza juhudi za Rais Samia hivyo Nkinda aliwarai wanafunzi wakawe mabalozi wazuri wa kazi zinazofanywa na rais hasa kwa upande wa elimu na kuboresha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi.
Aidha, alimpongeza kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi kupitia Mfuko wa Ufadhili wa Samia na kueleza kuwa mpango huo utaongeza ari ya wanafunzi wengi zaidi kujiunga na masomo ya sayansi.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo cha Ustawi wa Jamii, Chisanti Mutatina alisema kuongezwa kwa fedha ya kujikimu ni matokeo ya mwaliko walioupata kutoka kwa Rais Samia kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mazingira ya elimu.
Alisema katika mazungumzo yao walikuwa na maombi kadhaa likiwemo la kuongezwa fedha ya kujikimu ambapo kwa kutambua umuhimu wa wasomi Rais Samia aliona ni vyema alitekeleze.
Awali fedha ya kujikimu iliyokuwa ikitolewa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaopokea mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ilikuwa Sh 8,500, Rais Samia aliiongeza kufikia Sh 10,000.
Pia alimpongeza Rais kwa kuongeza bajeti ya fedha za mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka Sh bilioni 570 hadi bilioni 654 zilizowezesha wanafunzi wengi zaidi kupata mikopo kwa asilimia 100.