Biashara

SHIUMA yawashangaa Machinga kuchezea fursa

MLEZI wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) Salim Asas amewashangaa baadhi ya machinga wa mjini Iringa kwa namna wanavyochezea fursa iliyopo mbele yao inayolenga kuboresha mazingira yao ya biashara na kukuza mitaji yao.

Ameyasema hayo wakati shughuli za biashara za machinga katika soko lao la Mlandege zikizinduliwa katika hafla iliyohusisha chakula na vinywaji kwa wafanyabiashara hao zaidi ya 1000 na wageni wote waliohudhuria.

Kabla ya chakula, viongozi wa dini mbalimbali waliombea shughuli za kibiashara katika soko hilo ili zifanikiwe sambamba na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kifedha zikiwemo benki za NMB na CRDB zilitangaza fursa za mikopo ya masharti nafuu kwa wafanyabiashara hao.

“Tumejenga soko hili la Mlandege kwa gharama kubwa na bado halijakamilika. Wakati wadau tukijipanga kuliboresha zaidi ikiwa ni pamoja na kusakafia na kuweka huduma zingine zikiwemo za matangazo ya televisheni mbalimbali, bado kuna machinga wanasua kuhamia hapa,” alisema.

Pamoja na fursa za kibenki, Asas ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa alisema yeye binafsi alitenga Sh Milioni 50 kwa ajili ya machinga hao kujikopesha ili kukuza mitaji yao ambazo kati yake Sh Milioni 25 zilikwishatolea huku kiasi kilichobaki kikisubiri utayari wao baada ya kujipanga katika maeneo ya biashara kwenye soko hilo.

“Machinga wa Iringa watata sijapata kuona, wanataka siku zote wawe wachuuzi wa kutembeza biashara barabarani. Hawa ni sawa na wale wanaojenga nyumba lakini wanataka kulala jikoni badala ya chumbani,” alisema.

Alisema ili machinga hao wafikiwe na fursa hizo ni muhimu wakawa sehemu moja kama ilivyo makusudio ya soko hilo ambayo itatoa fursa nyingine ya kufikiwa na wateja wao kwa wingi zaidi.

Awali Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema muda wa machinga kusalia katika maeneo yasio rasmi umekwisha na akatoa wito kwa wote walioko huko kwenda katika soko rasmi la Mlandege kabla hawajafikiwa na mkono wa dola.

“Mambo yote ambayo machinga waliiomba serikali iyafanye kabla ya kuhamia katika soko hili la Mlandege yamekamilishwa kwa asilimia 99. Kwahiyo hakuna sababu inayowafanya waendelee kuwepo katika maeneo yasio rasmi,” alisema.

Ngwada alitoa msimamo huo baada ya Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, Matondo Masanja kuzungumzia jinsi machinga wa Iringa walivyodekezwa huku Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya SHIUMA, Jerry Mwatebela akiviomba vyombo vya dola kukaza uzi kwa machinga wanaopuuza maelekezo ya serikali.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button