Simulizi

SIMULIZI| KITUMBUA CHA KIHINDI SEHEMU YA – 05

Sehemu ya Tano (5)

“Kumbe?”

“Sina kipingamizi tena”

“Kipingamizi cha nini?”

“Nipo tayari kufanya biashara” Ashura alizungumza huku akiwa amemkazia macho zawadi usoni. Zawadi alitoa tabasamu lililoonekana wazi kuwa lilikuwa limejaa dharau na kebehi.

“Biashara gani?” alihoji Zawadi huku akijitikisa kwa nyodo.

“Ya kitumbua cha kihindi”

“Hata kama usingekuwa tayari ni lazima ungefanya tu” Zawadi alizungumza huku akiendelea kujitingisha tingisha na mikono yake ikiwa ingali kifuani.

“Ningefanya kivipi?”

“Unakumbuka kama ulikwisha kula kiapo cha kufanya kazi pamoja nasi?”

“Ah! hakukuwa na sababu ya kupeana viapo, ila kwakuwa imekwishatokea hakuna tatizo” alijibu Ashura kwa kujiamini.

Zawadi alichukua lile sinia la vitumbua na kuelekea nalo upande wa kushoto ambako Ashura hakuwahi kufika. Waliingia kwenye chumba kimoja kilichokuwa kimejaa brifkesi za kila saizi na kila rangi kwenye makabati.

Zawadi alichukua brifkesi ndogo na kuanza kupanga vile vitumbua. Ashura aliendelea kumsoma rafiki yake yule ambaye alikuwa akimfundisha kazi. Kitendo kile kilikuwa kigeni machoni mwa Ashura. Hakuwahi kuona vitumbua vinahifadhiwa kwenye brifkesi kama noti ama nguo.

Zawadi alipomaliza kupanga vitumbua vile kwenye ile brifkesi aliinua shingo kumtazama Ashura ambaye alikuwa amesimama pembeni yake akimtazama kwa makini.

“Unaona mzigo huu?” Zawadi alihoji huku ameinua ile brifkes kwa mkono wake wa kulia.

Ashura akaitikia kwa kichwa kuonesha kuwa alikuwa ameiona.

“Mzigo huu unathamani ya dola za kimarekani ‘Bilioni moja na ushee’” alisema Zawadi na kumfanya Ashura kushituka.

“Unasema!….”

“Habari ndio hiyo mama”

“Mnh! kwakweli wacha vijana wa kitanzania wanyongwe huko china” alizungumza Ashura huku ameweka kiganja cha mkono wake wa kuume kifuani.

“Wanaokamatwa ni wazembe. Sisi tuko vizuri mama” Zawadi akazungumza kwa kujiamini.

“Sasa huo mzigo unakwendaje sokoni?” Ashura alihoji kwa udadisi mkubwa.

“Huu unasafirishwa kwenye makontena ya vyakula kama vyakula vya kawaida”

“Haviharibiki?”

“Sio rahisi, ule unga umechanganywa na kemikali maalumu za kuzuia vyakula visiharibike hata kama vikikaa miaka kumi” alisema Zawadi.

“Duh! ama kweli mmekamilika” Ashuara alitamka.

“Si hivyo tu mama, mzee mwenyewe ameshikilia serikali hapa kiganjani” alisema Zawadi.

“Mnh! Serikali hii?” Ashura akahoji kwa kuhamaki.

“Wewe ukijua la kulia, wenzako wanahamia la kushoto”

“Unataka kusemaje?”

“Kila kukicha, mzee na kamati yake wanawaza mbinu za kujilinda na kuishi kwa usalama” Zawadi alieleza.

“Kwahiyo hatuwezi kukamatwa?”

“Tutakamatwaje sasa? Mwenyewe umeona kila siku watu wanashikwa lakini hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa kwenye mtandao wetu” Zawadi alieleza.

“Mnh, unaanza kunitia moyo” alisema Ashura.

“Tupo vizuri kila idara mama. Njoo huku nako uone mambo yetu” Zawadi alizungumza huku akiondoka na brifkesi ya vitumbua mkononi. Kama ilivyokuwa kawaida Ashura alimfuata kwa nyuma.

Waliingia sehemu moja iliyokuwa na kiuchochoro chembamba sana. Walipenya kwenye kiuchochoro kile kilichokuwa kirefu na kutokea sehemu moja iliyokuwa na mawe mengi makubwa. Juu kulikuwa na kitu kama tundu la darini.

Zawadi alipanda kwenye mawe na kudandia pale juu kama ngedere kisha akajivutia kwa ndani. Alipoingia aligeuka na kunyoosha mkono kwa Ashura ambaye alikuwa amesimama chini akimuangalia.

Ashura alinyoosha mkono wake na kuukamata mkono wa Zawadi. Alivutwa na kudondokea ndani mle.

Kilikuwa ni chumba kidogo mno kilichokuwa kimetawaliwa na kiza kinene. Zawadi alipowasha tochi wakaona ngazi iliyokuwa ikiteremka chini kwa upande mwingine.

“Twende huku” alisema Zawadi huku akiteremka ngazi zile.

Ashura alifuata nyuma bila kipingamizi chochote. Waliteremka ngazi nyingi sana “hadi walipokaribia kufika chini wakasikia sauti za watu wakizungumza kwa makelele.

“Nani hao Zawadi?” Ashura alihoji kwa wasiwasi.

“Vijana hao wapo kazini”

“Vijana?” Ashura akahoji kwa wasiwasi.

“Ndio vijana wa kazi” Zawadi alijibu huku akiendelea kushuka ngazi.

Mwanga wa taa uliokuwa ukitokea chini uliashiria kuwa safari yao ilikuwa imekaribia kufika ukingoni. Na dalili zilionesha kuwa kule walikokuwa wanaelekea kulikuwa na mwanga wa kutosha. Ashura akawa anatembea huku akikodolea macho yake mbele kwa hamu kubwa ya kuona kile kilichokuwa kinaendelea kule chini.


Hasira za Bi.Fahreen zilishindwa kuzuilika ndani ya moyo wake. Ghafla alijikuta akiwachukia vijana wale wawili yaani Magosho na binti yake Rachna. Sababu kubwa ya chuki ile ilikuwa ni mapenzi. Aliamini kwa asilimia zote kuwa binti yake Rachna alikuwa akitoka kimapenzi na asali wake wa moyo.

Bi.Fahreen alishindwa kufanya kitu chochote kile tangu Magosho alipoondoka nab inti yake. Alihisi viungo vya mwili vikimnyog’onyea na kukosa hamu ya kufanya jambo lolote lile. Alisogea kibarazani na kuketi huku akiona dunia ikizunuuka kutokana na wivu ulivyokuwa umemtawala. Alikumbuka bastola ya mume wake na kutamani kuitumia katika kuhakikisha Amani ya moyo wake inapatikana. Ndio, Bi. Fahreen alikuwa tayari kutoa uhai wa mtu ili kulinda Amani na furaha ya moyo wake.

Muungurumo wa gari waliyoondoka nayo Rachna na Magosho ulimgutusha kutoka kwenye lindi la mawazo. Baada ya sekunde kadhaa gari ile ilifunga breki hatua chache kutoka pale barazani alipokuwa amekaa Bi. Fahreen..

Mtoto Vashal aliteremka na kumkimbilia Bi.Fahreen kumkumbatia kwa furaha kama ilivyokuwa kawaida yake siku zote alipokuwa akitoka shuleni. Lakini siku hiyo mambo yalikuwa tofauti kabisa kwa mtoto yule kwani hakuchangamkiwa kama ilivyo kawaida ya mama yule.

“Mom tatizo iko nini?” alihoji mtoto Vashal kwa mashaka.

“Nenda ndani baba” alisema Bi.Fahreen.

“Mr.Nakesh iko piga veve?”

“Vashal, nenda kwa nyumba” alijibu mwanamke yule kwa ufupi.

“No Mom, nani chuza veve?” mtoto Vashal aliendelea kudadisi.

“Vashal mimi iko piga veve, I said nenda kwa nyumba!” Bi.Fahreen alizungumza kwa ukali na kumsukuma Vashal.

Mtoto Vashal alipofokewa na kusukumwa ikabidi ajiongeze na kutoka nduki kuingia ndani na kumuacha mwanamke yule aliyekuwa mkali kama mbogo pale barazani.

Vijana wale wawili walipoteremka tu Rachna alimsogelea Magosho na kumshika mkono, wakawa wanatembea huku wameshikana mikono. Bi.Fahreen alipowaona akasimama ghafla kutaka kuwavaa wawili wale waliokuwa wamedhamiria kuumiza moyo wake.

Bi. Fahreen alipokuwa akivuta hatua kuwafuata Magosho na Rachna alihisi kizunguzungu kikali kikimtawala na kushindwa kuhimili mikiki. Pumzi zilimuishia na kudondoka chini kama mzigo ‘Puuu!’.

“Gosooo help! help! faster” Rachna alimkimbilia mama yake na kumuinua shingo kisha akamuweka kwenye mapaja yake.

“Mom!…Mom!…..Iko nini tatizo?” Rachna alipaza sauti kumuita mama yake huku akiwa na wasiwasi na hofu kubwa. Hata hivyo Bi.Fahreen alionekana kuwa na hali mbaya kuliko mbaya.

Magosho na Rachna walisaidiana na kumpakia kwenye gari kisha zoezi la kuelekea Hospitali ilifanyika kwa haraka. Rachna alionekana kuchanganyikiwa baada ya kiona hali ya mama yake jinsi ilivyokuwa. Alikuwa akiwapenda sana wazazi wake na hakutamani kuwaona wakiteseka hata kidogo.

Kwa msaada wa Magosho, Bi.Fahreen alilazwa kwenye hospitali moja ya private iliyokuwa inafahamika kwa jina la ST.METHEW ambayo ilikuwa inapatikana maeneo ya Posta pale jijini Dar.

Baada ya masaa mawili hali ya Bi.Fahreen ilianza kutengemaa. Mr.Nakeshwar alikuwa pembeni yake akimliwaza mke wake kipenzi, laadhidhi wake nyonga mkalia ini. Rachna na Magosho hawakuwepo muda huwo.

“Hello my wife how are you?” (Vipi mke wangu unaendeleaje?) alihoji Mr.Nakeshwar kwa sauti iliyojaa upendo na huruma.

“Am fine my husband, what is going on?” (nipo vizuri mume wangu, vipi nini kinaendelea?) alihoji Bi.Fahreen kwa taabu huku akizunguusha macho yake kuangalia mazingira ya pale hospitalini.

“Just relax my lovely wife,I will inform you every thing letter” (Pumzika kidogo mke wangu, baadae nitakufahamisha kila kitu) alisema Mr.Nakeshwar kwa ile sauti yake ya kubembeleza.

Bi. Fahreen alijaribu kuvuta kumbukumbu lakini hakuweza kukumbuka juu ya kilichotokea hadi kufikia hatua ile ya kulazwa hospitalini pale, tena mkononi akiwa na drip la maji na glucose.

Baada ya dakika kadhaa Rachna alifika hospitalini pale akiwa ameongozana na Magosho. Kama ilivyokuwa kawaida ya Rachna kila alipokuwa anatembea alipenda sana kumshika mkono Magosho.

“Mom iko mapata nafuu?” alizungumza Rachna kwa furaha kubwa baada ya kumkuta mama yake amezinduka.

Kwa mapenzi aliyokuwa nayo binti Rachna kwa mama yake yule, akajikuta amepatwa na furaha ya kupitiliza. Alimfuata Magosho na kumkumbatia kwa lengo la kufurahia ahuweni aliyokuwa nayo mama yake kipenzi. Alimbusu Magosho kwenye mashavu yake mara kadhaa huku akicheka kwa furaha masikini ya Mungu. Hakika lilikuwa ni jambo la furaha na lililokuwa limejaa Baraka za Mungu.

Jamani jamani nyie! Kumbe kitendo kile cha Rachna kumkumbatia Magosho na kummiminia mvua ya mabusu kutokana na furaha, kilikuwa ni kitendo cha hatari sana kwa afya ya Bi.Fahreen. Hali ya Bi. Fahreen ikabadilika tena na kuwa mbaya, Alikuwa akipumua mfurulizo huku akitoa macho utafikiri alikuwa katika harakati za kuachanisha roho na mwili.

“Emergence! Call nurse” (mwite nesi kuna dharula) Mr.Nakeshwar alipaza sauti kuomba maada.

“N u r s e !….. N u r s e!…..Help…..N u r s e” Rachna naye alipaza sauti huku akikimbia kuelekea kwenye chumba cha manesi kuweza kupata msaada wa haraka.


Ashura aliendelea kuwa na hamu kubwa ya kuweza kufahamu kile kilichokuwa kinaendelea kule chini ya ngazi. Macho ya Ashura yaliweza kushuhudia chumba kilichokuwa na eneo moja pana sana.

Ashura hakuweza kuamini alichokuwa anakiona mbele ya macho yake katika eneo lile pana. Kulikuwa na vijana kama kumi na mbili hivi waliokuwa wameshiba kwa mazoezi ya viungo. Lakini walikuwa kama vile wanapigana kwa kurushiana ngumi na mateke mazito.

“Huuuu!….. Haaaa!….. Huuuu!…. Haaaa!” vijana wale walikuwa wakipiga kelele kila walipokuwa wakirushiana ngumi na mateke.

“Zawadi ni nini hiki, kwanini wanapigana?” alihoji Ashura kwa sauti ndogo lakini iliyokuwa imejaa hofu na mashaka.

“Shsss tulia! Hawapigani hawa wanafanya mazoezi” Zawadi akamtuliza Ashura kwa sauti ndogo na Ashuara akatii amri.

Wakasogea hadi sehemu moja ambako vijana wawili walikuwa wakipambana na mtu mmoja. Walipofika tu vijana wale wakaacha kupambana na kutoa salamu kwa Zawadi kwa kuinama kidogo na mikono yao wakiwa wameibandika kifuani.

Zawadi akanyoosha mkono kama vile alikuwa anaomba kitu Fulani kutoka kwa vijana wale. Mmoja wa wale vijana alimletea grops za kupigania, wenyewe sijui wanayaitaje, yale ambayo wanayavaa mkononi mabondia wakati wakapigana ulingoni.

Zawadi alivaa grops zile kisha akampa Ashura ishara ya kusogea pembeni, akawaita vijana kwa ishara huku akibonyea kidogo huku amekunja ngumi na miguu yake akiipishanisha kwa kuruka ruka kidogo. Vijana wote watatu wakakunja ngumi na kumsogelea Zawadi taratibu.

Ilikuwa ni kama vile picha ya kichina kwa Ashura kwani alishangaa shoga yake alivyokuwa akipambana na vijana wale walioonekana kushiba mazoezi. Vijana walijitahidi kurusha ngumi na mateke lakini Zawadi aliyaona na kupangua kisha akawa anawatwika yakwake takatifu. Baada ya dakika chache vijana wote watatu walikuwa chini hoi bin taaban. Hawakutamani kumsogelea tena zawadi.

Zawadi alimgeukia Ashura ambaye alikuwa angali kwenye mshangao. Alitoa tabasamu na kumkonyeza. Ashura alikuwa kama vile amegandishwa kwenye barafu. Hakujibu wala hakutikisika. Aliendelea kumshangaa rafiki yake yule ambaye siku hiyo alikuwa ameamua kumuonesha mambo ya kushangaza.

“Vipi unaweza?” alihoji Zawadi huku akitabasamu huku akivua zile gloves na kuzitupa pembeni.

Ashura aliendelea kumtazama pasipo kutikisika wala kuzungumza neno lolote lile. Nafikiri kati ya mambo yote aliyoyaona siku hiyo, lile la shoga yake Zawadi kupambana na wanaume watatu walioshiba na kuwashinda kilimshangaza zaidi.

“We Ashura!” Zawadi aliita kwa sauti huku akimpigia makofi karibu na usoni.

Ashura alishituka kama vile mtu aliye gutushwa kutoka usingizini. Zawadi naye akatulia akimshangaa rafiki yake kwa jinsi alivyokuwa.

“Kumbe ndivyo ulivyo?” alihoji Ashura kwa sauti ya tahadhari.

“Yeah, vipi unaweza?” Zawadi akahoji huku akijifuta jasho kwa taulo dogo lililokuwemo ndani mle.

“Mnh! sijui hata kukunja ngumi” Alijibu Ashura.

“Nenda bwana kidogo tuu ukajaribu!”

“Niende wapi, we Zawadi niende wapi?” Ashura alihoji huku ametoa amacho kwa msisitizo.

“Nenda ukanitwangie wale vijana wawili pale” Zawadi alizungumza huku akimuoneshea Ashura vijana wawili waliokuwa wakirushiana ngumi karibu na pale walipokuwa.

“We Zawadi wewe, Muogope Mungu!” alizungumza Ashura kwa msisitizo.

“Wale wachovu tu hawatakusumbua” Zawadi alizungumza huku akiachia tabasamu la masihara.

“Thubutu! Hunipeleki popote” Ashura akazungumza kwa msisitizo.

“Usijali utajua tu na pengine ukawa mkali kuliko hawa wote” Zawadi alizungumza huku akiwaoneshea kidole wale watu waliokuwemo mle ndani.

Ashura alizunguusha macho kuwatazama vijana wale waliokuwa bize na mazoezi.

“Sasa hawa nao kwanini wako hapa?”

“Hawa ni vijana wa bos Nakeshwar”

“Wao wanafanya kazi gani?”

“Hawa ni walinzi wa biashara zetu. Huwa hawachelewi kutoa uhai wa mtu mzembe ama anayejaribu kuingilia biashara zetu” alisema zawadi.

“Kwahiyo nawewe unaweza kuua?” Ashura akahoji kuhamaki.

“Kama kuna mtu atakayejaribu kunitia hatarini sioni dhambi kummaliza yeye kabla ya yeye kunimaliza mimi” alisema Zawadi kwa kujiamini.

“Mnh!”

“Usigune, hata wewe inabidi uwe vizuri kwaajili ya usalama wako kwasababu watu kama sisi tunasakwa kwa udi na uvumba na serikali mbalimbali hapa duniani” Alisema Zawadi kwa msisitizo.

Ashura alizidi kuona ugumu na uhatari wa biashara ile ambayo awali aliiona ni rahisi na salama. Akapumua kwanguvu kuashiria ugumu wa kazi.


Mr.Nakeshwar alikuwa amechanganyikiwa kutokana na kubadilika kwa hali ya mke wake. Akiwa nje alikuwa akitembea tembea hapa na pale. Alikuwa hajisikii kukaa wala kusimama. Daktari alikuwemo wodini akiendelea kumtibia mke wake kwa uangalifu zaidi.

Magosho alikuwa ametumwa kumpeleka Rachna benki kuchukua pesa kwaajili ya matibabu ya Bi.Fahreen. Hivyo wodini pale alikuwepo Mr.Nakeshwar pekeyake. Baada ya dakika kadhaa mlango wa wodi ile ulifunguliwa na Daktari akatoka.

“Vipi Dokta?” Alihoji Mr.Nakeshwar huku akiwa ametoa macho.

“Anaendelea vizuri mzee usihofu” Daktari alizungumza kwa upole.

“Naweza kumuona?”

“Anatakiwa kupumzika kwa muda mrefu” alisema Daktari kwa umakini mkubwa.

“No Dokta, ruhusu mimi maone muke yangu mara moya!”

“Ok. Nakupa dakika tano” Daktari alizungumza kisha akaondoka na kumuacha Nakeshwar akiingia wodini.

Bi.Fahreen alikuwa amerejewa na fahamu ingawa hali yake haikuwa ya kuridhisha.

“Muke yangu!” aliita Mr.nakeshwar.

Bi.Fahreen aligeuza shingo na kumtazama mume wake pasipo kutoa sauti yake.

“Vipi my wife?”

“Niko vizuri”

“Kwani tatizo iko nini muke yangu?”

“Rachna”

“Racha iko tuma kwa benki kuchukua some money”

“Goso?”

“Goso iko peleka Rachna kwa benki” Mr.Nakeshwar alieleza pasipo kufahamu kuwa maelezo yake yale yalikuwa yakimuumiza sana mke wake.

“My God!” Bi.Fahreen alizungumza huku akionekana kupoteza amani.

“Kwani iko nini my wife?”

“That is a huge mistake” (umefanya kosa kubwa sana) alisema Bi.Fahreen huku sura yake ikionekana kujawa na hofu kubwa.

“What mistake?” (kosa gani?)

“Goso is a problem” (Magosho ni tatizo)

“How?” (kivipi?)

“Goso iko tembea na Rachna” alitamka Bi.Fahreen kwa ghadhabu.

“What?” (nini?) Mr.Nakeshwar alihamaki.

“Yes, Goso iko chezea matoto yetu Rachna” Mwanamke yule aliendelea kutapika maneno ya uchonganishi.

“Are you sure?” (una uhakika?)

“Hundred percent” (asilimia miamoja)

“Shit! he must be perished” (shenzi! ni lazima afe) Mr.nakeshwar alizungumza huku akitetemeka kwa hasira.

Wakati mzee yule wa kihindi alipokuwa akitetemeka kwa hasira, simu yake ya mkononi iliita. Aliitoa mfukoni na kuitazama kujua mpigaji. Aligundua kuwa aliyekuwa anampigia alikuwa Mansoor yule mfanya biashara mwenzie.

“Hallo”

“Yes. Mr.Nakeshwar, Just come faster. Something is wrong” (Ndio Mr.Nakeshwar. Njoo haraka kuna tatizo kidogo) alizungumza Mansoor kwenye simu.

“Where?” (wapi?)

“Cerena Hotel”

“Ok. Five minutes” (Sawa. Nipe dakika tano) Alizungumza Nakeshwar na kukata simu. Alimtazama mke wake kwa sekunde kadhaa kisha akaondoka kwa haraka sana huku akili yake ikionekana kuvurugwa na taarifa za kijana Magosho kuwa na mahusiano ya kimapenzi na binti yake kipenzi Rachna.

Mr.Nakeshwar aliendesha gari kwa mwendo mkali sana. Baada ya dakika tano alikuwa amekwishafika kwenye hoteli ya Serena. Alipoingia tu hakupata shida kumtafuta Mansoor kwasababu alikuwa amekaa kwenye makochi ya pale ghrorofa ya chini. aliongoza moja kwa moja hadi pale alipokuwa ameketi.

“What is the matter?” (Kuna nini?) alihoji Mr Nakeshwar punde tu alipofika.

“Have a seat and calm down” (kaa chini halafu tulia) Mnsoor alizungumza kwa upole.

Mr.Nakeshwar alikaa kwenye kochi na kumsikiliza Mansoor kwa makini ingawa akili yake ikiwa imekwisha chafuka. Alichukia sana kwasababu Magosho alikuwa ni mswahili na wao walikuwa ni wahindi. Hivyo kutokea kwa kitu kama kile kilikuwa ni aibu kubwa sana kwenye familia ya tajiri kama yeye.

“Am sory Mr.Nakesh kwa hili nitakalokwambia. Sina jinsi” alisema Mansoor kwa utaratibu.

“Tafadhali ambia mimi bana kubwa” alisema Nakesh.

“Unafahamu kuwa yule dereva wa mke wako anakuzunguuka?” alizungumza Mansoor kwa umakini mkubwa na kumeza funda la mate.

Mr.Nakeshwar aliowanisha taarifa zile na maneno aliyokuwa ameambiwa na mke wake kule hospitali. Hasira juu ya Magosho ikaongezeka zaidi.

“Yes iko mapata taarifa” alijibu Mr. Nakeshwar huku akionekana kufahamu kila ambacho Mansoor alikusudia kumueleza.

“Umeambiwa na nani?”

“My wife” (Mke wangu) alijibu Mr.Nakeshwar.

“Mke wako?” Mansoor alihoji kwa mshangao huku ametoa macho kwasababu alichokuwa anataka kumuelewa isingewezekana Bi. Fahreen kuzungumza kwa mume wake.

“Yes, ingawa my wife iko gonjwa lakini ambia mimi majinga ya Goso” alizungumza Mr.Nakeshwar huku akiumauma midomo yake kwa hasira.

“Bado unanichanganya Mr.Nakeshwar. Unasema aliyekwambia ni nani?” Mansoor aliendelea kuchanganyikiwa na kuhoji kwa mshangao mkubwa.

“My wife Bi.Fahreen ambaye iko Hospital” alizungumza Mr.Nakeshwar huku akikuna nywele zake kwa hasira.

“Mnh! Huyo mke wako ameanzaje kukwambia jambo hili?” Mansoor alionekana kuzidi kuchanganywa na maneno ya Mr.Nakeshwar.

“That boy must die!” (Yule kijana ni lazima afe) alisema Nakeshwar kwa hasira.

“Sawa, niambie huyo mke wako amekuelezaje?”

“Fahreen told me that Goso iko fanya matoto yangu maakuli” (Ameniambia kuwa Magosho anatembea na binti yangu) alisema Mr.Nakeshwar kwa uchungu.

Taarifa zile zilimshangaza sana Mansoor. Taarifa alizokuwa anampa ni kwamba Magosho anatembea na mke wake. Sasa akashangaa kuwa kijana huyo huyo alikuwa na mahusiano ya kimapenzi tena na Rahna.

“Unamaana jamaa anakula kuku na watoto wake?”

“What do you mean Mansoor?” (unamaanisha nini Mansoor?)

“Ni dharau kubwa sana”

“Ni kweli lakini iko maanisa nini?”

“Ni aibu boss”

“Ambia mimi bhanaa!”

“Kwa ufupi ni kwamba huyo kijana anatembea na mke wako” alisema Mansoor kwa msisitizo.

“What!…Nasema nini?…..No!….No!….Hapana wezekana kabisa” Mr.nakeshwar aliinuka juu na kuzungumza huku mikono akiiweka kichwana na kuihamishia kiunoni kabla ya kuitumbukiza mfukoni.

“Tulia Bwana Nakesh” Mansoor alijaribu kumtuliza.

Mr.Nakeshwar hakumuelewa rafikiyake. Aliondoka kwa mwendo wa spidi kali sana na kumuacha rafiki yake amekaa akimtazama alivyokuwa akitokomea. Vijana wanakwambia kilikuwa kimenuka.


Mazoezi aliyokuwa akipewa Ashura na rafiki yake zawadi yalimfanya kuwa vizuri sana katika sekta ya mapambano. Jitihada alizokuwa nazo zilimfanya kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya vijana ambao alikuwa amewakuta pale kambini.

Ashura akiwa amezunguukwa na vijana sita wakipambana naye kimazoezi, Zawadi alikuwa pembeni akipanga mzigo wa vitumbua vyenye unga wa COCAIN ndani yake. Yalikuwa ni maandalizi ya kupeleka mzigo huwo nchini Afrika kusini.

Kwa kiasi kikubwa sana Ashura alikuwa ameweza kuimudu kazi ile na kuizoea sana. Hakuwa anajilaumu tena kama ilivyokuwa awali.

Lango kuu lilifunguliwa kwa mbwembwe na Mr.Nakeshwar akaingia. Watu wote wakiwemo Ashura, Zawadi pamoja na vijana wengine waligeuka na kumtazama. Sura ya Mr. Nakeshwar ilionekana kuto kuwa ya kawaida. Macho yake yalikuwa mekundu mno na mwili wake ulikuwa ukimtetemeka na vinyweleo vimemsimama. Zawadi akatazamana na Ashura kisha wakakonyezana kama ishara ya kupeana tahadhari.

Mr.Nakeshwar alizunguusha shingo kwenye jumba lile na kuwatazama vijana wake kwa hasira.

“Keje hapa yote” Mr. Nakeshwar alipaza sauti kwa hasira kuwakusanya vijana wake.

Vijana wote walisogea huku wakiwa wamejawa na wasiwasi kwenye mioyo yao. Hawakuzoea kumuona bosi wao akiwa katika hali kama ile. Ni kweli kabisa Mr. Nakeshwar alikuwa anakasirika lakini hakuwahi kufikia hatua ile.

“Afrika yote majinga jinga, kuje hapaaa!” Mr. Nakeshwar alipaza sauti kuzunumza kwa kufoka.

“You!” (wewe!) Mr.Nakeshwar alizungumza huku akionyesha kidole kwa Ashura na Zawadi.

“Yes Boss” Zawadi na Ashura waliitika kwa unyeyekevu huku wakionekana kuwa na hamu ya kutaka kufahamu sababu ya ujio wa bosi wao akiwa katika hali kama ile.

“I want some one to be ded by today” (Nataka mtu mmoja auwawe leo hii) alizungumza Mr.Nakeshwar huku akitetemeka kwa hasira na mate yakimtoka mdomoni kama matone ya mvua.

Zawadi akatazamana na Ashura kwa sekunde kadhaa kisha wakapeana ishara ya kutekeleza agizo lile la bosi wao.

“Ni kazi rahisi bosi” Ashura alizungumza kwa ukakamavu na kujiamini.

“Ni nani huyo mtu tumalize kazi bosi?” alihoji Zawadi.

“Hapana uliza swali nyingi bhanaa! Mimi iko taka maroho sasahivi” alizungumza Mr. Nakeshwar kwa hasira utafikiri waliosababisha hasira zile walikuwemo ndani ya mjengo ule.

Vijana waliposikia Maneno yale kila mmoja alijiweka sawa kwa kuchukua silaha yake na kuiweka kiunoni tayari kwa mapambano.

Mr.Nakeshwar aligeuka na kuanza kuondoka kwa haraka. Ashura alivuta hatua na kutaka kumfuata kwa nyuma lakini Zawadi akamdaka mkono na kumrudisha.

“Niachie mimi” alisema Zawadi kwa sauti ndogo.

“No! na mimi nina hamu ya kuua leo” Ashura alimjibu Zawadi kwa msisitizo.

“Hii kazi inaelekea ni ngumu Ashura, wacha nikamridhishe bosi” Zawadi alizungumza.

“Kwahiyo unataka kusema mimi siwezi kikazi?” Ashura akahoji kwa msisitizo.

“Unaweza Ashura, lakini tambua kuwa hujawahi kuua mtu wewe” Zawadi alieleza.

“Unafikiri nitaanza lini kama sio leo? Ngoja na mimi nikamthibitishie bosi kuwa niko vizuri kikazi” Ashura alizungumza kwa kujiamini.

ENDELEA…

“Ok utaua, lakini wacha mshenzi huyu nikammalize mwenyewe” Zawadi alizungumza kwa msisitizo.

“Basi twende sote” Ashura akatoa wazo.

“Hapana Ashura, wewe baki na kikosi kazi ukiandae kwaajili ya mapambano. Kama kazi itakuwa ngumu basi tutawafahamisha mje kutoa msaada mara moja” Zawadi alieleza.

“Lakini Zawadi…” Ashura alitaka kuzungumza kitu lakini kabla hajamaliza Zawadi alimkatisha.

“Hakuna cha lakini Ashura, Hii ni mbinu moja wapo ambayo tunaitumia katika wakati kama huu. Kuwa makini” alizungumza Zawadi na kuondoka haraka pamoja na vijana wengine watatu huku wakimuacha Ashura mwili wake ukichemka kwa hamu ya kutaka kuua. Roho yake ilikuwa imekwisha mbadilika na kusikia harufu ya damu ya binadamu imemtawala kwenye tundu za pua yake. Alirusha ngumi kwa hasira na kupiga ukuta. Aliamini kuwa hakuwa ametendewa haki na rafiki yake kwa kukatazwa kwenda kufanya mauaji yale kwa mkono wake.


Kule hospitali kwa Bi.Fahreen, Rachna na Magosho walikuwa wamejawa na furaha baada ya kumuona mama yao amerejewa na fahamu kwa mara nyingine. Rachna akiwa ameketi kwenye kitanda alichokuwa amelala Bi.Fahreen, Magosho alikuwa amekaa kwenye kiti kidogo pembeni mwa kitanda kile. Mkono wa kulia wa Bi.Fahreen ulikuwa kwenye viganya vya mikono ya Magosho vikisuguliwa suguliwa taratibu.

Kitendo cha Magosho kumsugua sugua Bi.Fahreen kiganja chake cha mkono kilimfanya mama yule kuhisi hali fulani ya ahuweni ndani ya moyo wake. Hata hivyo alipopeleka macho kumtazama binti yake Rachna alihisi dukuduku kubwa limemkaba moyoni. Alitamani kumrukia na kumrarua kwa meno lakini hakuwa na uwezo huwo masikini ya Mungu. Jamani nyie acheni tu, mapenzi haya!

Rachna hakuelewa chochote kilichokuwa kikiendelea baina ya mama yake na dereva wao Magosho. Alichokuwa anakijua yeye ni kwamba Magosho kuchua mkono wa Bi.Fahreen hakikuwa kitu kibaya kwasababu ni kama mtu na mwanawe. Hata hivyo Magosho alikuwa ameushika mkono wa Bi.Fahreen kwa lengo la kumfariji kama mama yake mzazi na si vinginevyo.

Bi.Fahreen alikuwa akijitahidi kukwepesha macho yake kumtazama binti yake na badala yake muda mrefu aliyatuliza macho yake usoni mwa Magosho. Alihisi damu zikitereza kwenye mishipa yake kiulaiini. Alitamani sana wasaa ule wangekuwa wenyewe wawili tu maeneo yale ili apate angalau busu kutoka kwa kijana yule aliyetokea kuukonga mtima wake. Akainua macho yake na kumtazama binti yake.

“Rachna” Aliita Bi Fahreen kwa sauti kavu lakini iliyokuwa imelegea kutokana na kitendo cha Magosho kumsugua sugua kiganja cha mkono wake.

“Yes Mom” Rachna aliitika kwa heshima na bashasha.

“Nenda kwa home letea mimi majuisi” (Nenda nyumbani ukaniletee juisi) alisema Bi.Fahreen pasipo kumtazama Rachna usoni.

“Oh! Juisi ya nini Mom?” alihoji Rachna kwa hamasa. Alifurahi sana kusikia mama yake alikuwa anahitaji kula.

“Pinaple” (Juisi ya Nanasi) Bi.Fahreen alijibu kwa ufupi.

Rachna aliinuka kwa hamasa kubwa na kumshika Magosho begani.

“Twende basi Goso” alizungumza Rachna kwa sauti ya kutokea puani kama vile mgonjwa wa mafua.

Bi.Fahreen aliposikia maneno ya binti yake alihisi maumivu makali mithili ya mtu aliyekuwa amechomwa mkuki kwenye moyo wake. Alifumba macho kwa sekunde kadhaa kuyasikilizia maumivu yale kutoka moyoni na kuenea sehemu mbalimbali za mwili wake. Racha akagundua utofauti aliokuwa nao mama yake.

“Whats rwong Mom?” (Nini tena mama?) Rachna alihoji huku akimsogelea haraka sana mama yake na kumuwekea kiganja cha kushoto shavuni.

“No thing wrong, just go” (hakuna kitu we nenda) Bi.Fahreen alizungumza huku akiutoa mkono wa binti yake kutoka kwenye shavu lake.

“Ok, Goso subiria mimi hapa” Rachna alizungumza na kuondoka huku akiamini amemuwacha Magosho kuhakikisha usalama wa afya ya mama yake kipenzi.

Rachna alipowapa kisogo tu Bi.Fahreen alikunja sura na kuvuta midomo yake kwa nyodo na hasira kuonesha wazi kumchukia binti yule aliyewahi kuishi ndani ya tumbo lake la uzazi kwa takribani miezi sita.

“Kwanini unafanya hivyo Bi.Fahreen?” Magosho alihoji Baada ya kugundua kuwa Bi.Fahreen hakuwa sawa kwa binti yake.

“Shut up!” Bi.Fahreen alipaza sauti kwa Hasira kumtaka Magosho anyamaze.

Magosho akatii amri na kukaa kimya. Alikuwa akimtazama mke wa bosi wake kwa macho ya tahadhari.

“Veve Goso tazama mimi?” Bi. Fahreen alizungumza kwa jazba.

Magosho aligeuza shingo na kuangalia pembeni huku mikono yake ikiwa ingali imekamatia kiganja cha mama yule wa kihindi.

“Kwanini veve iko matesa mimi?” alihoji kwa hasira Bi. Fahreen.

“Kwani nimefanya nini mama?”Magosho akahoji kwa umakini mkubwa.

“Kwanini veve iko magawa penzi kwa matoto yangu Rachna?” alihoji mama yule kwa umakini.

“Mnh mama! Mbona hakuna kitu kama hicho” Magosho akazungumza kwa mshangao. Ni kweli kabisa hakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti wa mama yule pamoja na uzuri aliokuwa nao.

“Sasa baba ya matoto yangu iko jua kila kitu” Bi Fahreen alizungumza kwa sauti ya msisitizo.

“Lakini mama hakuna kitu kinachoendelea kati yangu mimi na Rachna, tunaishi kama kaka na dada tu na hakuna cha zaidi” Magosho alijaribu kuzungumza ukweli mbele ya mwanamke yule aliyekuwa anaugua ugonjwa wa wivu.

“Kama iko kweli matembea na matoto yangu au hapana kweli, leo veve kufe” Bi. Fahreen alizungumza huku akijaribu kuchomoa mkono wake kutoka kwenye vianja vya Magosho bila ya mafanikio kwasababu Magosho aliuzuia mkono ule.

“Hapana jamani mnanionea bure mimi, hata sijawahi kumtongoza dada Rachna mimi” masikini Magosho aliendelea kujitetea kwa msisitizo.

“Mimi penda veve Gosoo lakini veve umisa mimi. Ondoka hapa mara moya, Mr. Nakeshwar kuje toa roho yako saa hii” Bi. Fahreen alizungumza kwa tahadhari kwasababu alikuwa akimfahamu vyema mume wake. Hakuwa na masihara kwa kibwengo yeyote yule aliyethubutu kuchezea maisha ya binti yake Rachna. Kitu kibaya zaidi ni kwamba bwana huyo alipata taarifa kuwa Magosho huyo huyo alikuwa akidokoa asali ya mtima wake.

Ghafla mlango wa wodini ulifunguliwa kwa nguvu na Mr.Nakeshwar aliingia huku akiwa ameongozana na watu wane akiwemo Zawadi na vijana wengine watatu.

Magosho alishituka na kuuachia mkono wa Bi.Fahreen haraka. Mr.Nakeshwar hakuweza kuamini macho yake kwa kile alichokuwa amekikuta pale. Yale aliyokuwa ameyasikia kutoka kwa rafiki yake Mansoor yalithibitika moja kwa moja. Hakuona sababu ya kuuliza.

“The dog is that one” (mbwa mwenyewe ni huyo hapo) Mr. Nakeshwar alizungumza kwa hasira huku akinyoosha kidole kwa Magosho.

Zawadi alisogea hadi pale kwa Magosho na kumuonesha ishara ya kuinuka kwa kidole chake cha kati huku amemkazia macho kijana yule.

Magosho alishangazwa sana na tukio lile lililokuwa likiendelea mbele ya macho yake. Alikuwa anamfahamu vizuri sana Zawadi. Msichana yule alikuwa wamekulia katika mtaa mmoja na kipindi cha utotoni walikuwa wakicheza pamoja. Pia alimfahamu Zawadi kwasababu alikuwa ni shoga mkubwa wa mdogo wake Ashura. Mara nyingi walipokuwa sokoni wakiuza vitumbua walipenda kukaa pamoja. Kwa ufupi ni kwamba alishangazwa sana na kuona msichana yule akiwa ameongozana na Mr. Nakeshwar. Mbaya zaidi alikuwa akimuonesha dharau. Magosho alitaka kuhoji kitu.

“Shssss” Zawadi alimnyamazisha kwa kuweka kidole mdomoni mwake na kumtolea macho kwa ukali zaidi.

Magosho alitii amri na kunyamaza kimya huku katika akili yake akiwa amejawa na maswali yaliyokosa majibu.

Zawadi akaonesha msisitizo wa kumuamuru Magosho kuinuka pale alipokuwa ameketi. Pasipo kujishauri alijiinua kwa kusitasita huku moyo wake ukiwa umejawa na wasiwasi pamoja na hofu.

“Usitucheleweshe we kunguni” Zawadi alizungumza huku akivuta hatua kumkaribia Magosho.

Zawadi alivuta mkono wake wa kushoto na kumtandika Magosho kofi moja takatifu sana maeneo ya shavuni karibu kabisa na shingoni. Magosho aliinama na kuweka mkono kwenye shavu kusikilizia maumivu ya pigo lile murua.

Dharau ile ilimuumiza sana Magosho, aliinuka na kurusha ngumi nzito kwa Zawadi lakini mwanamama yule aliiona na kuinyaka ikiwa hewani kabla haijatua kwenye pua yake ambayo ilikuwa imelengwa kung’olewa na Magosho. Haraka sana Zawadi alijibu shambulizi lile kwa kurusha ngumi yake ikamtwanga Magosho shavuni. Magosho alipepesuka na kudondokea kwenye kitanda alichokuwa amelala Bi.Fahreen.

“Uuuwiiiii!” Bi.Fahreen alitoa ukulele wa woga kama vile yeye ndiye aliyekuwa amepokea pigo lile kutoka kwa Zawadi.

“Kimya, Malaya kuba veve, iko ona raha tembea penzi na matoto dogo!” Mr.Nakeshwar alipaza sauti kumwambia mke wake. Kauli ile ilitosha kumfanya Magosho kutambua sababu ya hukumu ile aliyokuwa akipewa na mtoto wa kike.

Zawadi alimfuata Magosho pale kitandani akamshika shingoni na kumvuta juu. Alimuinamisha na kumtandika vigoti vitatu mfurulizo vya usoni. Magosho kama mtoto wa kiume hakutaka kushindwa kirahisi namna ile. Aliinuka na kumvaa Zawadi kwa hasira. Zawadi alimpisha na kumsukuma kwa teke takatifu la mgongoni. Magosho akapepesuka hadi alipokuwa amesimama Mr. Nakeshwar.

Mzee yule wa kihindi alimsukumia Magosho kwa baunsa wake ammoja ambaye alikuwa amesimama pembeni. Baunsa yule alitanua mikono yake na kuikutanisha pamoja kwa nguvu sana, akabana kichwa cha Magosho katikati ya mikono ile.

“Mama N a k u f a a a a !” Magosho alitoa ukulele wa maumivu makali yaliyotokana na kichapo kile. Sauti za ajabu ajabu zilikuwa zikisikika kwenye masikio yake. Machoni alikuwa akiona vitu Fulani fulani vilivyokuwa vikikatiza huku vikiwakawaka na kuzima kama nyota za mbingu ya saba.

“Kufa Malaya mkubwa wewe, unafaida gani duniani hapa!” alizungumza Zawadi huku akitoa bastola kutoka kiunoni na kuitoa loki tayari kwa kumsindikiza binadamu ahela.

Bi.Fahreen ambaye alikuwa ni mgonjwa mahututi pale kitandani alishituka sana baada ya kubaini kumbe adhabu ile aliyokuwa akipatiwa Magosho ilikuwa ni kwasababu yake. Alielewa wazi kuwa mwanaume yule wa kihindi asingeweza kumuwacha salama hata yeye. Akahisi kuwa baada ya Magosho zamu yake ilikuwa inafuata.

Mwanamke yule wa Kihindi aliinuka kutoka pale kitandani na kuchomoka kama mshale. Nakeshwar na vijana wake walijaribu kumshika lakini mama yule aliwatereza mikononi mwao mithili ya kambale kwenye tope na kufanikiwa kutoka nje.

Vijana wa Nakeshwar walitoka nje kwa lengo la kumkamata mama yule wa kihindi lakini bahati ilikuwa kwa Bi. Fahreen kwani alijipakia kwenye bodaboda na kumuamuru dereva kuondoka haraka. Waliondoka kwa mwendo mkali sana na kuwaacha vijana wale wakishangaa shangaa.

“Mazubaa nini veve? Fuata roho ya mbusi ile!” Sauti ya Mr.Nakeshwar ilisikika ikitoa amri kutokea kwenye mlango wa wodi ile.

Wakati vijana wale wakichukua pikipiki kwa waendesha bodaboda ghafla walishuhudia ile pikipiki iliyokuwa imembeba Bi. Fahreen ikiingia kwenye gari moja ya zima moto amabayo ilikuwa ikiendeshwa kwa spidi kuwahi huko ilipokuwa inaelekea.

Ilikuwa ni ajali ya kuogofya sana mbele ya macho ya binadamu. Bi.Fahreen alirushwa juu na kupeperuka mithili ya kipande cha karatasi. Alipotua chini kichwa kilitangulia na kukipiga kwenye lami ‘Paaa!’.

Ndugu msomaji sijui niandike nini lakini ukweli ni kwamba kishindo kile kilipelekea kichwa cha Bi.Fahreen kupasuka na kumwagika damu nyingi sana. Najisikia vibaya sana kuandika lakini ubongo wa Bi.Fahreen ulikuwa umetapakaa barabarani. ‘Ina Lilahi Waina Ilaihi Rajiun’. Bi Fahreen alikuwa ameaga duania palepale.

“Hey kuje huku” Mr.Nakeshwar aliwaamuru vijana wake warudi ndani kushughulika na Magosho kwani adhabu aliyokuwa ameipata mwanamke yule ilikuwa inamtosha. Alionekana kuto kujali hata kidogo kwa kile kilichokuwa kimetokea barabarani pale. Jmani nyie kuna watu ni makatili, Duu!

Kule ndani Magosho alikuwa akiendelea kupokea kichapo kutoka kwa Zawadi pamoja na baunsa mmoja. Mr.Nakeshwar aliamuru Magosho atolewe nje. Kilikuwa ni kitendo cha haraka. Magosho alitolewa na kupakiwa kwenye Pajero moja nyeusi ambayo ilikuwa imeongozana na msafara ule wa Mr.Nakeshawar.

Wakati Magosho alipokuwa anaingizwa kwenye gari ile Rachna alikuwa ndio anaingia maeneo yale. Alishangazwa sana na tukio lile lililokuwa likiendelea mbele ya macho yake. Aliteremka kwenye gari na kuelekea kwenye gari lile haraka. Haikuwa rahisi kuweza kufika eneo lile kwani magari yale yaliondoka kwa mwendo wa kasi na kumuacha Rachna akiyatazama kwa mshangao.

Msichana Rachna alipotupa macho upande wa kulia aliona kundi la watu barabarani. Hakutaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea maeneo yale. Aliingia wodini na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba alichokuwa amelazwa mama yake. Alishituka sana baada ya kukuta kitanda kikiwa kitupu. Akatoka nje pasipo kuhoji mtu akaingia kwenye gari yake na kuondoka haraka kuwafuata wale ambao walikuwa wameondoka na Magosho.

Rachna alipokuwa akiingia barabnarani alishangazwa na kile alichokuwa anakiona mbele ya macho yake. Mwili wa Bi.Fahreen ulikuwa umelazwa pembeni ya barabara. Alifunga breki kwa ghafla na kuteremka. Alikwenda hadi pale kupata uhakika wa macho yake. Ni kweli mama yake mzazi alikuwa ameaga dunia. Rachna naye akadondoka chini na kupoteza fahamu.


Ashura alikuwa peke yake kwenye chumba cha mazoezi akijifua tayari kwa kufanya mauaji ya binadamu ambaye alikuwa amemuudhi bosi wake Mr.Nakeshwar. Alikuwa akirukaruka mithili ya kangaroo pale ndani. Kila dakika alikuwa akiangalia saa yake ya mkononi na kuona Zawadi na bosi wake walikuwa wanachelewa kumletea huyo binadamu ambaye angekuwa ni wa kwanza kumtoa roho kwa mikono yake. Ingawa hakuwa amewahi kuua lakini alijishangaa sana siku ile kwa jinsi ambavyo alikuwa na hamu kubwa ya kupoteza uhai wa binadamu mwenzake.

Sauti ya lango kuu likifunguliwa ilimgutusha Ashurana na kutoka nje kushuhudia kilichokuwa kinaendelea. Aliwaona wale vijana wa Mr.Nakeshwar wamemshikilia mtu huku kichwani wakiwa wamemfunika kwa kipande cha gunia.

Ashura alipomuona binadamu yule alivuta pumzi ndefu na kumeza funda la mate ya uchu. Mwili wake ulikuwa ukitetemeka kwa hasira. Alisogea kwa kasi sana eneo la tukio na kurusha ngumi kali ambayo alikuwa amekusudia kumtwanga binadamu yule maeneo ya usoni lakini Zawadi alijirusha juu akatua mbele ya Ashura na kuidaka ngumi ile amabayo ilimyumbisha kidogo.

“Zawadi unafanya nini sasa!” Ashura alipaza sauti kwa hasira baada ya ngumi yake kuzuiwa na Zawadi kufanya shambulizi lile maridadi.

“Punguza jazba mjeshi wangu, huyu ni wako” Zawadi alizungumza kwa sauti ya chini lakini iliyokuwa imejaa umakini mkubwa.

“Sasa kama ni wangu kwanini unanizuia nisifanye kazi yangu?” Ashura alilalama.

“Nakuzuia kwasababu ni wako!” Zawadi na yeye alizungumza kwa hasira na msisitizo mkubwa.

Maneno ya zawadi yalimtia hasira Ashura na kumfanya arushe ngumi kwa zawadi lakini Zawadi aliidaka ngumi ile na kumkunja mkono.

“Maji hayawezi kupanda mlima hata siku moja ndugu” alizungumza Zawadi huku midomo yake ameibinua kwa dharau.

Ashuara alichomoa mkono wake kutoka kwa Zawadi na kujivuta nyuma hatua chache.

“Hata kama wewe ndiye uliyenifundisha kupambana lakini huwezi kunizingua” alisema Ashura huku akiwa amekunja ngumi kutaka kupigana na Zawadi. Alichokuwa amekibaini ni kwamba Zawadi alikuwa anamzuia kujinyakulia taji la ushujaa na mauaji.

Zawadi hakuwa amekunja ngumi kama ambavyo alifanya Ashura. Yeye alikuwa akimtazama tu rafiki yake yule kama vile video.

“Naelewa hujui ufanyalo, nimekusamehe” Zawadi alizungumza na kuvuta hatua kutaka kuondoka lakini Ashura alimrukia kwa nyuma na kumtandika teke la kiunoni. Zawadi aligeuka kwa hasira na pasipo kujishauri alirusha mkono na kutuma kofi zito kwenye shavu la Ashura. Kofi lile lilimfanya Ashura kupepesuka marakadhaa hatua chache kutoka pale alipokuwa amesimama Zawadi. Alipokuja kutuliza akili yake alishangaa zawadi akimkabidhi silaha.

‘Yanini?” ashura alihoji.

“Chukua we si unataka kuua!” Zawadi alizungumza kwa msisitizo.

“Sihitaji silaha yoyote, nataka kuua kwa mikono yangu” Ashura alizungumza kwa kujiamini. Zawadi akacheka kidogo na kutikisa kichwa kwa masikitiko.

“Huwezi kupambana na mimi pasipokutumia silaha” alisema Zawadi kwa kebehi.

“Sina shida ya kupambana na wewe” Ashura akajibu.

“Huwezi kutamani kupambana na mimi ikiwa unafahamu wazi kuwa huniwezi kupambana na mimi” Zawadi alizungumza.

“Hata kama ningekuwa na uwezo wa kupambana na wewe, kamwe nisingethubutu, hiyo niliyokuonesha ilikuwa ni changamoto tu” Ashura alizungumza.

“Unadhani ni kwanini usingeweza kupambana na mimi?” Zawadi alihoji.

“Wewe ni ndugu yangu kabisa, tena huna tofauti na kaka yangu Magosho” Ashura alizungumza kwa msisitizo. Maneno hayo yalimfanya Zawadi kuangua kicheko kwa dakika kadhaa.

“Haya twende ukaue dada wa damu” Zawadi alizungumza na kumshika mkono Ashura.

Walielekea kwenye chumba cha mateso. Walipofika chumbani pale Zawadi akasimama pembeni na kumtaza Ashura jinsi ambavyo alikuwa akitetemeka kwa hamu kubwa ya kutaka kupoteza uhai wa binadamu mwenzie.

“Think twice before” (Fikiri mara mbili kabla ya kufanya kitu) alizungumza zawadi.

“Achana na mimi” Ashura alijibu huku akisogea pale alipokuwa amefungwa Magosho.

Alifunua kile kipande cha gunia ili kuweza kumuona binadamu yule kabla ya kumteremshia kichapo. Waswahili wanasema damu ni nzito kuliko maji. Macho ya Ashura yalikumbwa na kigugumizi baada ya kumuona mtu yule. Alikuwa ni kaka yake Magosho ambaye alizaliwa naye tumbo moja.

“Kill him” Zawadi alizungumza kwa msisitozo lakini kwa sauti ya chini.

Ashura alirudi nyuma hatua kadhaa na kumgeukia zawadi. Alikuwa haelewi kilichokuwa kikiendelea pale ndani.

“Vipi we si una hamu ya kuua?” Zawadi alihoji kwa msisitizo.

“Tatizo nini zawadi?” Ashura alihoji kwa upole huku mzuka wote ukiwa umetoweka hafla.

“Kama ulivyo wewe, hata mimi pia sifahamu” Zawadi alijibu.

“Hapana lazima kifanyike kitu hapa” alisema Ashura kwa msisitizo mkubwa.

“Kitu gani?”

“Magosho hawezi kufa mbele ya macho yangu”

“Okay fanya hicho unachoweza sasa, mbona unachelewa?” Zawadi akazungumza kwa msisitizo.

Vishindo vya miguu ya Mr.Nakeshwar vilisikika vikitembea kuelekea kule chumbani. Ashuara alikimbilia mlangoni na kujibanza kwa nyuma. Zawadi alisogea kwa Magosho na kumtandika ngumi mbili mfurulizo za kwenye tumbo. Magosho akatoa kelele kali za maumivu ambazo zilimfikia Mr.Nakeshwar kule nje.

Mlango wa chumbani mle ulipofunguliwa tu Ashura alimrukia nakeshwar na kumkaba shingoni. Mzee yule wa kihindi alikukuruka na kufanikiwa kubabadua roba ya binti yule na kumsukuma Ashura kwa nguvu. Akasogea nyuma hatua mbili na kusimama kwa mshangao. Hakuwahi kufikiria kama ingetokea hata siku moja kijana wake mwenyewe kumjaribu.

Ashura aliserereka na kujizuia kwa kukita nyuma mguu wake wa kushoto. Alikunja ngumi kwaajili ya kupambana na Mr. Nakeshwar. Binti yule alikuwa tayari kufanya chochote kuhakikiha maisha ya nduu yake Magosho yananusurika.

Vijana wengine wa Mr. Nakeshwar waliinua silaha zao tayari kwa kummaliza Ashura ambaye alikuwa anajaribu kutishia uhai wa bosi wao.

“No wacha!” Mr. Nakeshwar alitoa amri.

Wale vijana wote walishusha silaha zao chini kama ambavyo Bosi wao aliwaamuru.

“Zawadi nini hiki?” alihoji Mr. Nakeshwar kwa mshangao mkubwa.

Zawadi alibenjua mabega yake juu kuashiria kuwa hakuwa anafahamu kilichokuwa kinaendelea ndani mle kutokana na kile kitendo cha Ashura.

“Hey, cheza nayo!” alizungumza M.Nakeshwar huku akichagua kijana mmoja apambane na Ashuara.

Yule kijana alitii amri ya bosi wake na kuruka juu kama kiwavi kwa lengo la kumtandika Ashura teke la kifuani lakini binti yule alimuwahi kabla hajatua chini alibetua teke lile na kumzawadia ngumi moja nzito usoni kwenye mpaka wa jicho na shavu. Kijana yule alidondoja chini kama zigo na kushikilia shavu lake kwa mkono wa kushoto. Hakuwa na hamu tena ya kumsogelea binti yule aliyekuwa amejiunga na chama muda mfupi tu uliopita.

“Subiria nini veve pambana!” Mr.Nakeshwar alizungumza kwa ukali kuamuru vijana wengine wapambane na binti yule aliyebadilika ghafla na kuleta vurugu katika himaya yake.

Ndugu msomaji, Ashura alikuwa ameiva katika masuala ya masumbwi. Vijana wale wawili walivyokwenda walijikuta wakipokea dafrau moja matata kwa pamoja na kudondokea karibu na miguu ya Mr. Nakeshwar.

“Pumbavu veve, toto dogo iko sumbua nini bhanaa!” alizungumza Mr.Nakeshwar kwa hasira kisha akainua macho yake kumtazama Ashura ambaye alikuwa amekunja ngumi kusubiria vijana wengine.

“Suraaa, iko patwa manini yeo veve toto?” alihoji Mr. Nakeshwar.

“Bosi, naomba umwache Magosho aondoke” alizungumza Ashura kwa msisitizo.

“What! Iko taka nini veve?” Mr.Nakeshwar alihamaki baada ya kusikia maneno yale kutoka kwa binti yule aliyekuwa chini ya himaya yake.

Zawadi alimsogelea Magosho pale alipokuwa amefungwa na kumtandika ngumi tatu mfurulizo za kifuani kiasi cha kupelekea kijana yule kutoa kelele kali za maumivu.

Ukelele ule wa Magosho ulizidi kumtia wazimu Ashura kutokana na hasira zilizokuwa zikibubujika kwenye mishipa yake ya homoni. Alijituma kwa kasi sana akiwa na lengo la kwenda kubandika teke kwenye kifua na ngumi kwenye pua ya Mr. Nakeshwar. Laa haula! Alitokea Zawadi ghafla katikati na kuzuia shambulizi lile. Ashura akayumba na kudondoka chini kwa kutua na mgongo. Hatimaye nay eye alikuwa ameonja kile alichokuwa akikigawa kwa vijana wengine walithubutu kumsogelea kwa shari.

Zawadi alikuwa amesimama huku amekunja ngumi kwa hasira. Siku hiyo alikuwa amekusudia kumfunza adabu binti yule.

“Zawadi naomba ukae mbali” Ashura alizungumza akiwa pale chini ameshikilia kiuno chake kutokana na maumivu makali aliyoyapata baada ya kutandikwa na rafiki yake kipenzi Zawadi.

“Wewe ndio ukae mbali na Bosi. Vinginevyo nasambaratisha ubongo wako leo” Zawadi akajibu huku akirejesha mguu wa kushoto nyuma na kupeleka wa kulia mbele akiwa bado amekunja ngumi na macho ameyakodoa kwa binti yule mtata.

Ashura alijiinua kutoka pale chini kwa kuruka sarakasi na kusimama hatua chache kutoka alipokuwa amesimama Zawadi. Wawili wale wakawa wakikodoleana macho kwa mbinu za kishujaa huku kila mmoja akiwa amekunja ngumi.

“Zawadi kill that fullish dog!”(Zawadi muue huyo mbwa mshenzi) alizungumza Mr.Nakeshwar kwa hasira.

Ashura aliposikia maneno ya Mr. Nakeshwar alipata wazo la kumuwahi Zawadi kabla ya kumalizwa kweli. Alirusha teke kumpiga Zawadi shingoni lakini Zawadi kwa uhodari wake alizuia kwa mkono na kubetua mguu wa Ashura ambao ulikuwa umekita chini. Mguu ule ulifyatuka kama mtego na kujikuta akirushwa juu na kutua chini kwa kiuno.

“Hilo ni kosa kubwa, siku nyingine usirushe teke na mguu umeukita chini utakufa” Zawadi alizungumza kwa sauti ya upole huku akimsubiri Ashura ambaye alikuwa anajizoazoa kutoka pale chini.

Ashura alijiinua na kukung’uta viganja vya mikono yake kama vile alikuwa anafuta vumbi. Akakunja ngumi tena kujibu mashambulizi dhidi ya shiga yake kipenzi ambaye ndiye aliyekuwa mwalimu wake katika kazi ile.

“Tumia fursa hii vizuri vinginevyo itakula kwako” alizungumza Zawadi kwa sauti ya chini.

“Nyamaza shetani wewe!” Ashura alizungumza kwa hasira na kujizunguusha hewani kama feni huku amguu mmoja ameukunja na mwingine ameunyooka mbele kwa lengo la kushusha kipigo kwa shoga yake yule ambaye walikuwa wakiishi kama ndugu wa damu.

Mwalimu ni mwalimu tu ndugu msomaji, Zawadi aliweza kucheza na feni ile kwa kuikutanisha pamoja mikono yake na kuitanua ghalfa Ashura alipomfikia. Ashura akajikuta akizunguushwa zaidi na kutulizwa kwenye kifua cha Zawadi huku shingo yake imepigwa roba moja takataifu. Zawadi akampiga busu Ashura kwenye shavu lake la kuume kuashiria dhara.

“Finish her!”(Mmaliza huyo!) Mr.Nakeshwar akapaza sauti kwa ghadhabu.

“Nakupa nafasi ya mwisho shoga, ukiichezea hii tusilaumiane” alizungumza Zawadi kwa kumnong’oneza Ashura sikioni.

“Achana na mimi!” Ashura alizungumza kwa kiburi na kuvuta kisukusuku kwa mkono wake wa kulia na kumtandika Zawadi kwenye kidevu.

Zawadi alijikuta akimuachia Ashura na kupepesuka huku akishikilia kidevu chake kutokana na maumivu makali aliyoyapata. Alitema mate pembeni kuhakikisha kama hapakuwepo na jino ambalo limeng’olewa kutokana na pigo lile.

Wakati Zawadi akiendelea kuugulia maumivu yale huku machozi yakimlengelenga kutokana na maumivu makali, Ashura alimvamia shoga yake yule kama vile alikuwa anataka kufanya mapambano lakini alichomoa bastola kutoka kwenye kiuno cha Zawadi na kumgeukia ghafla Mr. Nakeshwar akamtandika risasi tatu mfurulizo ambazo mbili zilimpata kifuani na moja kwenye paji la uso.

Kilikuwa ni kitendo cha kushangaza sana machoni mwa Magosho ambaye muda wote alikuwa ametulia akishuhudia picha lile lililokuwa likichezwa na mdogo wake kipenzi.

Ashura aliteremsha mikono yake iliyokuwa imeshikilia bastola ile taratibu na kugeuza shingo yake kumtazama shoga yake Zawadi ambaye alikuwa amesimama akimkodolea macho kushuhudia jinsi mauaji yale yalivyokuwa yakiendelea.

“Umeridhika sasa, maana ulikuwa na hamu kubwa ya kuua!” Zawadi alizungumza kwa kuhamaki.

“Nashukuru kwa msaada wako” Ashura alizungumza kwa upole.

“Hongera kwa kuokoa maisha ya kaka yetu” Zawadi akajibu huku akikung’uta mikono kama vile amemaliza kazi nzito.

Ashura akamsogelea Zawadi na kumkumbatia kwa nguvu huku akitoa machozi ya furaha.

“Hakika wewe ni ndugu yangu wa damu” Ashura alizungumza kwa uchungu huku akimkumbatia kwa nguvu Zawadi.

“Hapa sio mahali salama tena Ashura tuondoke, kitumbua kimeingia mchanga” alizungumza Zawadi huku akivuta hatua kuelekea pale alipokuwa amefungwa Magosho na haraka sana akaanza kufungua Kamba.

“Pole sana kaka Magosho, nilifanya yote yale ili kuokoa maisha yako. Vininevyo ungeuwawa kabla hata hujafikishwa humu?” Zawadi alizungumza huku akifungua Kamba kwenye mikono ya Magosho.

“Hivyo mlivyo msitikisike wala kujisogeza” ilisikika sauti nzito ikiwaamuru kutokea kwa nyuma yao.

Nduu msomaji huwezi kuamini, kundi kubwa la watu waliokuwa wamevalia sare za jeshi la Polisi walikuwa wamewavamia huku wameshikilia silaha tayari kwa mapambano.

“Sisi ni jeshi la polisi na kuanzia sasa mpo chini ya ulinzi” Ilisikika sauti iliyokwaruza ikiwaamuru watu wote chumbani mle.

Ashura, na wale vijana wa Mr.nakeshwar wakainua mikono juu kuashiria kuwa walikuwa wamekubaliana na amri waliyokuwa wamepewa na jeshi la polisi.

Idadi kubwa ya askari ilikuwa imezunguuka jumba lile la Mr.Nakeshwar na kuliweka chini ya ulinzi. Rachna ambaye alikuwa ameambatana na askari wale alimfuata Magosho na kumkumbatia.

“Pole sana Goso mimi jua iko sababisa yote hii” alizunumza Rachna huku akimiminika machozi.

“Usijali Rachna nimekwisha poa”

“Goso mimi taka oa veve” Rachna alizungumza maneno yale ambayo yalimfanya Magosho kuhisi halifulani ya ubaridi kwenye mishipa yake ya damu. Akiwa amezubaa Rachna alipeleka midomo yake kwenye lipsi za kijana yule na kizibana na lipsi za midomo yake.

“Gosooo!” aliita Rachna kwa sauti kavu.

“Ndio Rachna” Magosho akaitikwa kwa upole.

“Mimi ndiye leta Polisi hii hapa” alisema Rachna.

“Kwanini umefanya hivyo Rachna?”

“Mimi maona Baba yangu mateka veve pale kwa hospital” Rachna alieleza.

“Okay nashukuru kwa msaada wako” Magosho akazungumza kwa upole.

“But Bi. Fahreen is ded!” (Lakini Bi.Fahreen amefariki) Rachna alizungumza kwa uchungu mkubwa huku akimwagika machozi.

“Mungu wangu! Unasemaje Rachna?” Magosho akahamaki baada ya kupokea taarifa ile ya kifo cha kipenzi chake, bosi wake, mwalimu wake wa udereva na mama wa Rachna mrembo aliyetokea kumpenda pamoja na kwamba hakuwahi kumueleza ukweli.

“Yes Mom iko pata maajali wakati baba fukuza yeye kwa bunduki. Mimi hapana penda tena baba yangu, bora yeye akufe nibaki mapekeyangu kwa dunia!” Rachna alizungumza kwa jazba na uchungu mkubwa wa kumpoteza mama yake kipenzi kutokana na ukatili wa baba yake Mr.Nakeshwar.

Magosho alipumua kwa nguvu na kumeza funda la mate kisha akamkazia macho Racha usoni.

“Inamaana ukikutana na baba yako unaweza kumuua?” alihoji Magosho kwa umakini mkubwa huku akimkazia macho usoni binti yule.

“Mimi hapana weza ua mamtu ya Mungu lakini kama iko mutu naua yeye hapana sida?” alizunumza Rachna kwa ghadhabu kubwa.

“Una uhakika na hilo?” Magosho akahoji tena kwa umakini.

“Gosooo, mimi iko tayari toa mapesa mingi baba akufe!” Racha akazungumza kwa msisitizo na ujasiri wa hali ya juu.

“Racha” Maosho akaita kwa utulivu.

“Gosoo mimi poteza mama yangu kwa sababu ya baba jinga jinga” alisema Rachna kwa uchungu.

“Baba yako amefariki” alisema Magosho kwa sauti ya msisitizo lakini iliyokuwa imejaa ukakasi.

“What! Goso iko sema nini veve?” Rachna alizungumza kwa kuhamaki huku akikusanya shati la magosho maeneo ya kifuani na kumtikisa kwa nguvu.

“Mr. Nakeshwar, ameuwawa na watu wake” alijibu Magosho kwa umakini wa hali ya juu.

“Hapana wevekana, baba yanu mimi hapana kufe Goso hapana hapana!” Rachna alionekana kuchanganyikiwa baada ya kupata taarifa ile ya kifo cha baba yake.

“Lakini Rachna baba yako si ndiye aliyehusika na kifo cha Bi.Fahreen?” Magosho akahoji kwa umakini akiwa na lengo la kupunguza machungu ya Rachna.

“Hata kama Goso, baba yangu ni baba yangu! Kama yeye kufe mimi Iko baki na nani hapa kwa dunia?” Rachna alihoji kwa Jazba huku akimtikisha Magosho kwa nguvu nahasira.

Kabla Magosho hajazungumza neno lolote lile msichana Rachna aliishiwa nguvu na kudondoka chini. Alikuwa amepoteza fahamu kutokana na mshituko wa taarifa zile alizozipata siku hiyo.

Magosho aliumia sana lakini angefanya nini, kufa kwa Mr. Nakeshwar ndio ilikuwa pona yake. Kama mzee yule wa kihindi asingeuwawa basi kifo kile kilikuwa ni cha halali yake. Tena kingekuwa ni kifo cha mateso makubwa sana.

Askari walipekuwa ndani ya jumba lile na kukuta idadi kubwa ya madawa ya kulevya ambayo mengine yalikuwa yamekwisha pakiwa kwenye vitumbua kwaajili ya kusafirishwa kwenda sokoni Afrika ya kusini na China.

Magosho hakuweza kuelewa kilichokuwa kinaendelea ndani mle kiasi cha kukutana na mdogo wake yule akiwa na ujasiri wa kuweza kutoa uhai wa binadamu mwenzake kwa urahisi kiasi kile.

“Ashura tatizo nini?” Magosho alihoji kwa umakini mkubwa.

“Kaka nakupenda sana lakini sina jinsi ni lazima tuachane. Mimi napaswa kufungwa kwa makosa makubwa mawili. Lakwanza ni kuua na la pili ni kujiingiza kwenye biashara haramu ya madawa ya kulevya.” Ashura alizungumza kwa machungu.

“Kwanini Ashura, Kwanini umefanya yote hayo?” Magosho alizungumza kwa uchungu huku akimkumbatia mdogowake.

“Nimefanya yote haya kwaajili ya maisha yangu mimi na wewe” alijibu Ashura huku akibubujikwa na machozi.

Askari walifika na kumchukua Ashura kutoka mikononi mwa Magosho. Wawili wale wakaachiana huku kila mmoja akionekana kuumizwa sana na tukio lile.

“Kaka KITUMBUA CHA KIHINDI kimetutenganisha leo” Ashura alizungumza huku akisukumwa na askari mmoja wa kike na kutolewa nje ya jengo lile.

Magosho akabaki akijutia sana yale yote aliyokuwa akiyafanya na mke wa bosi wake. Aliamini kuwa mambo yote yale yalikuwa yamesababishwa na yeye kwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa bosi wake. Imefikia hatua ya kumtia matatizoni mdogo wake kwasababu ya ile tabia yake mbaya. akaapa kuto kurudia tena mambo kama yale. Machoziyalikuwa yakitiririka utafikiri bomba la maji ya DAWASCO limepasuka.

Askari waliwachukua Magosho na Rachna kwaajili ya kuwapeleka hospitali kupata huduma za kiafya. Hali ya Magosho haikuwa nzuri sana kutokana na kipigo alichokuwa amekipokea siku hiyo.

“KITUMBUA CHA KIHINDI kimeniponza” Alizungumza Magosho kwa uchungu mkubwa uliokuwa umechanganyikana na majuto ndani ya nafsi yake. Alikumbuka maagizo aliyokuwa amepewa na mama yake kumlea na kumtunza mdogo wake vizuri. Akajiona ni mkosaji kwa kushindwa kutekeleza usia ule wa mama yake, akapeleka mikono yake usoni na kulia kwa kwiwi huku akiumia ndaniya moyo wake.

MWISHO!

Said Abdullah

^ SENIOR C E O & PUBLISHER ^ Software engineering ^ Fan of programming ^ Technology Enthusiast.. ^ System developed|C,C++&java 👇Get more news and updates

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button