Habari

Surua yaua 12, jamii yatakiwa kuzingatia chanjo

Watoto 12 walio chini ya umri wa miaka mitano Wilaya ya Mlele mkoani Katavi wamefariki kutokana na ugonjwa wa surua, huku watoto 646 wakiwa wameambukizwa ugonjwa huo katika kipindi cha kuanzia Desemba 2022 hadi Februari 2023.

Taarifa hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Dk, Wilaya ya Mlele, Martin Lohay katika mkutano wa hadhara uliofanyika kitongoji cha Bula Kata ya Majimoto.

“Mlipuko huu ulitokea mwezi wa 12 na kwa mara ya kwanza wagonjwa wengi walionekana kitongoji kinaitwa Mwamatiga kipo Kata ya Mbede, tulichukua sampuli 5 tukazipeleka maabara ya Taifa na zikagundulika kwamba ni ugonjwa wa surua,”amesema.

 

Martin Lohay,Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe

Katika kuhakikisha watoto wananusurika, serikali wilayani humo ikiongozwa na timu ya wataalamu imepanga kuweka kambi katika Kata zilizoathirika lengo likiwa ni kutoa elimu na kuwapatia chanjo watoto ili kuwakinga na ugonjwa huo na kwamba hadi sasa chanjo 2000 kutoka Wizara ya Afya zimepokelewa kati ya chanjo 40,000 zinazohitajika.

Mkuu wa Wilaya ya Mlele Majid Mwanga amesema moja ya jitihada zilizochukuliwa mbali na kupokea chanjo za kutosha, pia wamepeleka gari kila Kata litakalofanya kazi ya kuwazungusha wataalamu nyumba kwa nyumba kutoa elimu na kutoa chanjo kwa watoto kuanzia umri wa miezi 6 mpaka miaka 5.

Amesema utafiti umebaini kuwa, wanawake walio wengi wanajifungulia nyumbani badala ya vituo vya afya pamoja na baadhi ya wazazi kukatisha dozi ya chanjo ya kukinga ugonjwa wa surua.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha imani potofu kuwa vifo hivyo vinasababishwa na imani za kishirikana, bali wajikite kusikiliza maelekezo ya wataalamu kwa kuwa chanzo cha vifo hivyo ni kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo.

 

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button