Habari

TLS kuwasilisha mapendekezo Tume Haki Jinai

CHAMA cha Wanasheria nchini (TLS), kimesema kitawasilisha mapendekezo yake kwa Tume ya Haki Jinai, ili kufanya mabadiliko katika taasisi za haki jinai baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi zaidi ya milioni tatu.

Miongoni mwa mapendekezo waliyoainisha ni pamoja na kuundwa kwa chombo huru kitakachosimamia Taasisi za Haki Jinai, makosa yote yapatiwe dhamana ili kupunguza msongamano kwenye mahabusu na watu wasikamatwe kabla ushahidi haujakamilika.

Akizungumza leo katika kongamano lililohusisha wadau mbalimbali nchini, Meneja Programu wa TLS , Mackphasan Mshana alisema  mapendekezo hayo ni pamoja na mamlaka zinazofanya uchunguzi kujihakikishia kuwa mtuhumwa aliyekamatwa awe ndiye muhusuka.

“Tuko hapa kwa ajili ya kongamano la wazi, kuangali namna ya kuboresha taasisi za mfumo wa haki jinai nchini na Rais Samia aliunda tume iliyoanza kazi 31 Januari,2023 na imeshaanza kukusanya maoni.

“Tunapendekeza ili hizi taasisi zisifanye wanavyotaka kuwe na chombo huru kinachowafatilia namna wanavyofanya kazi na endapo kuna ukiukwaji wa haki waadhibiwe ,” alisisitiza.

Mshana amesema TLS  ni wadau muhimu, kwani jukumu lao ni kusaidia serikali na taasisi zake kuangalia mifumo yote ya kisheria na mifumo inayosimamia sheria  kwamba inaendana na matakwa, ambayo wanayo na inaendana na utawala wa kisheria.

“Sasa tumewiwa kuandaa kongamano hili kwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali, ili waweze kutoa maoni nini kifanyike,” amesema.

Amebainisha kuwa maoni yatakayotolewa na kukusanywa  yatasaidia tume kuandaa mapendekezo ambayo yatapelekwa ngazi ya serikali kwa ajili ya maboresho.

“Tumefanya kongamano la wazi kwa sababu kumekuwa na malalamiko kwa taasisi ambazo zinahusika katika mfumo wa haki jinai jinsi unavyofanya kazi, hasa taasisi zinazosimamia sheria kama mahakama, polisi, magereza, TAKUKURU,  dawa za kulevya,”ameeleza.

Amesema Kumekuwa na malalamiko kuwa kesi zinachukua muda mrefu, watu wanabambikiwa kesi, mtu anakamatwa kabla uchunguzi haujafanyika anakaa mahabusu muda mrefu, hivyo  wanataka kulinda mfumo huo.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button