Habari

TMA yatabiri kipupwe cha baridi ya wastani

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya msimu wa kipupwe katika kipindi cha Juni hadi Agosti 2023 ambacho kinatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani katika maeneo mengi ya nchi.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a juzi ilieleza kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa kuwepo katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini -Magharibi pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria huku vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Juni.

Alisema katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa Victoria (mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) wanatarajia kuwepo kwa hali ya baridi ya wastani hadi joto la kiasi. Dk Chang’a alisema kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 na 19.

Kwa Ukanda wa Pwani ya Kaskazini ambayo ni mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Dk Chang’a alieleza kuwa hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi.

Kwa mujibu wa Dk Chang’a, kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 22 na 26 kwa maeneo ya mwambao wa Pwani na visiwani na kati ya nyuzi joto 19 na 22 katika maeneo ya nchi kavu. Hata hivyo, alisema maeneo yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 19.

Alisema kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki yaani mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 na 21.

Taarifa hiyo ilisema katika maeneo yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 13 na pia Kanda ya Magharibi kwenye mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 na 19.

Dk Chang’a aliongeza kuwa Kanda ya Kati ambayo ni mikoa ya Singida na Dodoma hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14 na 19.

Kwa Ukanda wa Pwani ya Kusini, mikoa ya Mtwara na Lindi alisema hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 16 na 22 wakati Kanda ya Kusini katika Mkoa wa Ruvuma akieleza kuwa hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11 na 16.

Vilevile kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini-Magharibi inayohusisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya Kusini ya Mkoa wa Morogoro alisema hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto saba na 16. Kwa mujibu wa Dk Chang’a, katika maeneo ya miinuko kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto saba.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button