
IMANI za kishirikina zinaelezwa kuwazuia wanawake kushiriki katika shughuli za kuvua samaki kwenye maziwa na bahari, hivyo shughuli hiyo kulazimika kufanywa na wanaume pekee.
Mtafiti kutoka chuo kikuu cha Sokoine Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi, Profesa Anna Sikira alisema hayo akitoa taarifa ya matokeo ya awali ya utafiti ambao kituo hicho kimefanya juu ya usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika shughuli za uvuvi uliofanywa kwenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.

(Picha zote na Fadhili Abdallah)
Profesa Sikira ambaye ni Mkurugenzi wa kituo hicho, amefanya utafiti huo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa uvuvi kwenye Mwambao wa Ziwa Tanganyika (FISH 4 ACP) unaotekelezwa na kufadhiliwa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO).
Kutokana na hali hiyo Mtafiti huyo alisema kuwa sehemu kubwa ya wanawake wanabaki kuwa wamiliki na wachakataji, ambapo utafiti unaonesha kuwa asilimia 78 ya wachakataji wa mazao ya uvuvi kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika ni wanawake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wavuvi mwambao wa Ziwa Tanganyika, Francis Kabula amekiri kuwepo kwa vitendo vya kishirikina kwa baadhi ya wavuvi na kubainisha kwamba hiyo inatokana na kushindwa kujikita kwenye imani za kidini.
Mwenyekiti huyo amekiri kuwa kumekuwa na ubaguzi na unyanyapaa kwa wanawake kuingia ziwani kuvua kutokana na hali ya kuwa kwenye siku zao za hedhi kuonekana kama mkosi wanapojishughulisha na shughuli za uvuvi.
Akizungumzia kufanyika kwa utafiti huo Mratibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), Hashim Muumin alisema kuwa utafiti huo unalenga kubaini changamoto, fursa na kutengeneza mpango ambao utawezesha kuinua ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uvuvi.

Muumini alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uvuvi haupo kabisa na sehemu kubwa imebaki kuwa wamiliki, wachakati na wauzaji wa mazao ya uvuvi kuliko kuingia ziwani na kwamba mradi huo unalenga na kuongeza kipato kwa watu wote wanaojishughulisha na uvuvi na mazao ya uvuvi.