Habari

Ummy aridhishwa na mwenendo wa MSD

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu ameeleza kuridhishwa na mwenendo wa Bohari ya Dawa (MSD) katika kutekeleza majukumu yake kwa kutaka kila mmoja kutimiza wajibu wake ili taasisi hiyo iendelee kufanya vizuri.

Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imepongeza kile ilichosema inaona yapo maboresho na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye bohari hiyo.

Hayo yalielezwa juzi wakati kamati hiyo ya kudumu ya bunge ilipotembelea ofisi za MSD Kanda ya Dodoma kushuhudia majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na taasisi hiyo ya serikali.

“Naanza kuona matumaini kwa MSD kwamba tunakwenda vizuri, tutakwenda sasa vizuri endapo kila mtu atatimiza wajibu wake,” alisema Ummy baada ya taasisi hiyo, kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai kuwatembeza wabunge na kuwaelezea shughuli za bohari.

Akielezea masuala mbalimbali ikiwamo changamoto zinazokabili bohari, Ummy alisema miongoni mwa mambo yanayosumbua ni eneo zima la maoteo ya bidhaa za afya ambalo baadhi ya halmashauri huisingizia MSD kuchelewesha dawa wakati wao ndio wenye upungufu.

“Wakienda wakubwa, ameenda rais, makamu wa rais au waziri mkuu, unasikia mtu anakuambia tunadai MSD wakati kumbe hakupeleka maombi ya dawa…kwa sababu kuna kujificha kwenye kivuli cha MSD kumbe kuna wengine hawajapeleka hata hayo maoni,” alisema na kuongeza kuwa angependekeza kila zahanati kuwa na mfamasia.

Kuhusu uteketezaji dawa zilizoisha muda wake, Ummy alisema kwa mwananchi, linaweza kuonekana ni jambo kubwa lakini kitaalamu, inaruhusiwa dawa zilizoisha muda wake, thamani yake isizidi asilimia tano ya fedha.

“Kwa hiyo mpaka dakika hii, hatujafikia hiyo asilimia… tumefikia asilimia 1.1. Mtu wa kawaida anaweza asikuelewe, lakini tutatoa majibu,” alisema na kuongeza kwa kutoa mfano kwamba kwenye dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs), zilibadilishwa na kutumia aina nyingine.

Hata hivyo, Ummy alisema hoja yake ni kuhusu uteketezaji dawa hizo kwa wakati kama ilivyo kwenye hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) za ripoti ya mwaka 2022/2023. Aliitaka bohari ya dawa kuhakikisha dawa zilizoisha muda wake, hazikai muda mrefu bila kuteketezwa.

Katika hatua nyingine, Ummy ameelekeza MSD kuanzia sasa kununua maji ya dripu kutoka viwanda viwili vya uzalishaji ambavyo vimeihakikishia serikali kuwa na uwezo wa kukidhi soko la ndani. Viwanda hivyo vya dawa ni cha Kairuki na Alfa.

Vilevile Ummy alihimiza umuhimu wa kuifumua Bohari ya Dawa kimuundo ikidhi mahitaji ya majukumu yake hususani baada ya kuongezwa jukumu la uzalishaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo alisema kazi wanayoifanya MSD ni kubwa, inayohitaji utaalamu wa hali ya juu.

Alisema utunzaji dawa, ununuzi na usambazaji si sawa na bidhaa nyingine. “Tunatambua jinsi mnavyopambana… Kwa niaba ya kamati na wabunge, tunachokiona sasa hivi kuna maboresho na mafanikio makubwa yaliyopatikana. Tunawashukuru na kuwapongeza.”

Nongo alisema wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, wataendelea kuipima taasisi hiyo kwa jambo moja ambalo ni upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya na hospitali.

Alisema wabunge wataendelea kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha kuwa mikakati inayopangwa na MSD inaendelea kutekelezwa kukabili changamoto za upatikanaji dawa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kuhusu muundo wa utumishi kutokana na kuongezwa jukumu la uzalishaji, Nyongo alishauri MSD ikae, itulie na ije na muundo halisi utakaokidhi majukumu yote.

Akirejelea mada iliyowasilishwa kwa wabunge ikionesha kuwa ili bohari iweze kuzalisha vyema inahitaji Sh bilioni 593 ikiwamo uzalishaji unaohitaji Sh bilioni 92, mwenyekiti wa kamati alihoji endapo fedha hizo zinatosha.

Alimshauri waziri kufanya upembuzi yakinifu kwenye uzalishaji na kuitaka kamati ipewe mchanganuo mzuri ili isaidie kuomba serikalini hatimaye taasisi ifikie malengo mazuri ya uzalishaji.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button