HABARI

Usikilizwaji kesi ya kina Mbowe wakwama kwa muda

By James Magai

By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Usikilizwaji wa kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake wawili umekwama kwa muda baada ya wanachama na wafuasi wa Chadema kugomea masharti yaliyowekwa na mahakama kwa watu wanaotaka kuingia ukumbini kusikiliza kesi hiyo.

Mbowe na wenzake—Halfani Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdilkahi Ling’wenya wanatuhumiwa kujihusisha makosa ya ugaidi na uhujumu uchumi.

Kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021 inasikilizwa katika Mahakama Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.

Miongoni mwa masharti yaliyogomewa ni kutoingia na simu katika chumba cha mahakama.

Pia mahakama imetoa utaratibu mpya wa kuingia mahakamani hapo leo ambapo mawakili 20 wa utetezi, mawakili wa serikali nane, ndugu wa washitakiwa wasiozidi watano, viongozi watano, watu wa ulinzi na usalama watano, wanahabari 10 na watu maalumu watatu ndio watakaoruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa mahakama.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mustapha Siyani likuwa imepangwa kuendelea leo Alhamisi Septemba16, 2021 kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Advertisement

Mpaka sasa kesi hiyo haijaanza kusikilizwa ingawa washtakiwa walikuwa wameshaingizwa mahakamani pamoja na mawakili wa pande zote. Wakati wakimsubiri jaji, tangazo likatolewa likiwataka watu wote kutoka nje na wabaki washtakiwa tu.

Baada ya watu wote kutolewa nje wakiwamo washtakiwa ambao walirudishwa mahabusu, hakuna taarifa yoyote ya nini kinachoendelea au kinachofuata.

Kwa sasa, hata waandishi ambao awali walikuwa wameruhusiwa kuingia na simu wametakiwa waache nje.

This article Belongs to

News Source link

Publisher

Swahili Publisher , Publishes swahili articles in this website
Back to top button