Biashara

Utekelezaji Mradi Umeme wa Maji Kagera waiva

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wametoa mkopo wa Sh bilioni 374.9 za utekelezaji wa mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono uliopo mkoani Kagera. Mradi huo utazalisha megawati 87.8 za umeme na kuingiza kwenye gridi ya taifa.

Akizungumza leo Machi 15, 2023, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema serikali iliiomba AfDB na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kufadhili mradi huo ambapo kwa pamoja AfDB, AFD kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya na Tanzania zikakubali kuufadhili mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 750.

Amesema Machi 7, 2023 serikali ya Tanzania ilitia saini mkataba na AFD ya sehemu yake ambayo ni Euro milioni 110 sawa na takriban Sh bilioni 272.6 na kuwa jana mdau wa pili ambao ni AfDB nao wamesaini mkataba wa mkopo kwa sehemu yao wa shilingi bilioni 374.9.

“Kwa hatua hii tumebakiza kusaini mkataba wa msaada na Umoja wa Ulaya (EU) wenye thamani ya Euro milioni 35 sawa na shilingi bilioni 86.7 bilioni,mategemeo yetu ni kwamba nao watasaini mapema ili utekelezaji wa mradi huo uendelee kama ilivyopangwa,”alisema Dk Mwigulu.

Akizungumza mradi huo na manufaa yake, Dk Mwigulu alisema Kanda ya Ziwa imekuwa ikipata umeme wake kutoka kwenye mitambo ya kufua umeme kwa kutumia nishati ya dizeli ambayo ni ya gharama kubwa na hiyo imefanya kanda hiyo kutokuwa na nishati ya uhakika.

Katika kutatua changamoto hizo, serikali iliiomba AfDB na AFD kufadhili mradi na wakakubali na sasa utekelezaji wake unakwenda kuanza .

Alisema utekelezaji wa mradi huo utakamilika ndani ya miaka mitano na utahusisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme na kazi nyingine ni ujenzi wa shule ya msingi, kituo cha afya pamoja naujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 28.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button