
BAADHI ya wakulima wa mazao mbalimbali likiwemo zao la muhogo katika Halmashauri ya Mji wa Newala mkoani Mtwara uchumi wao umeanza kuimarika baada ya kushauriwa na serikali kulima mazao mengine tofauti na korosho.
Wakizungumzia jitihada zinazofanywa na serikali wilayani humo, wakulima wa zao hilo ambao kwa sasa wamehamasika kulima kilimo hicho wamesema wameanza kuona faida kubwa ya kulima mazao mchanganyiko tofauti na ilivyokuwa awali.
Mkulima aliyefahamika kwa jina la Mariamu Machemba amesema jitihada hizo zimeleta tija kubwa kwao kutokana kipato katika familia zao kimeongeza zaidi ikilinganishwa na hapo awali kipindi wanalima zao moja tu la Korosho.
‘’Kwa sasa faida kubwa tunazipata kwasababu kipato kimeongezeka na kimekuwa endelevu baada ya kufanya kilimo mbadala nasaidia familia yangu kama kusomesha Watoto na kuendesha majukumu mengine na nawashukuru sana Wataalam wetu wa kilimo katika halmashauri yetu wamekuwa mstari wa mbele kunipa ushauri wa kitaalam’’,
Ahmadi Kandembe mkulima wa zao la muhogo ‘’Nawashauri wakulima wenzangu wasiangalie sana zao moja tuu tujitahidi tuweke mazao mchangayiko mfano hili la muhogo kitatusaidia kuwa na uchumi/kipato endelevu’’,
Alisema, kilimo hicho cha mazao mchanganyiko gharama ya uendeshaji wa shamba imekuwa ndogo ikilinganishwa na kilimo cha korosho ambapo ni miaka mitatu sasa analima kilimo cha mazao hayo mchanganyiko na kuelezea namna ambavyo hivi sasa zao la muhogo lilivyokuwa na soko nzuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo awali walikuwa wakilima kiasi kidogo kwa ajili ya chakula tu lakini sasa wanalima kama zao la biashara.
‘’Sasa hivi zao la muhogo lipo vizuri mfano mwaka huu tumeuza muhogo kwa bei kubwa sana tofauti na miaka yote tumeuza kiloba cha kilo 100 kwa bei ya Shilingi 70 elfu mpaka 80 kwahiyo muhogo bado uko vizuri zaidi na miaka ya nyuma tulikuwa tunauza Shilingi 25 elfu mpaka 30 elfu lakini mwaka huu umefanya vizuri na Watu wengi kwa sasa wameanza kulima zaidi sana muhogo ’’,Alisema Kandembe
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Mji Newala Shamimu Daudi amesema wameamua kubadilisha mfumo na kuhamasisha Wananchi kulima kilimo hicho cha mazao mchanganyiko kama vile muhogo na mengine na Wananchi hao wamehamasika na kilimo hicho kinaendelea vizuri.
‘’Kama halmashauri tumehasisha wananchi wajihusishe na kilimo mbadala na sasa tunavyozungumza wananchi wengi wamehamasika kulima mazao hayo mchanganyiko”