Habari

Waliokufa ajali ya basi Katavi watajwa

MGANGA Mkuu Wilaya ya Tanganyika, Dk Alex Mrema ametaja majina ya watu saba kati ya tisa waliokufa katika ajali ya basi la Komba’s katika mlima Nkondwe kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Dk Mrema alitaja marehemu hao ni Anisia Kapandila (52), Anthonia Kapandila (27), Edigar Gilidas (1.5), Eva Sylvanus (40), Eliud Mashaka (10), Beka Mashaka (8) na toa Nzikwi (30).

Alieleza kuwa miili ya marehemu wawili ilikuwa haijatambuliwa. Marehamu hao tisa waliagwa juzi katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Watu hao akiwamo mjamzito walikufa na wengine 30 walijeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka na kutumbukia bondeni katika mlima wa Nkondwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame alisema ajali hiyo ilitokea juzi alasiri wakati basi hilo aina ya Tata lenye namba T 506 DHH liitwalo Komba’s lilipotumbukia kwenye bonde hilo.

Ilidaiwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa breki na kusababisha basi hilo kukosa mwelekeo na kuporomoka bondeni umbali wa mita 75.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko alisema serikali imeguswa na ajali hiyo na akatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waliopoteza maisha.

Mmoja wa majeruhi katika ajali hiyo, Philbert Focus, mkazi wa Mpanda alisema walipofika katika mlima huo kwenye kona gari lilienda kwa kasi kubwa kama limekatika breki likamshinda dereva na kupitiliza hadi bondeni.

 

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button