Habari

Wapongeza huduma matibabu ya moyo Zanzibar

WAKAZI wa Zanzibar wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma ya upimaji na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima, inayotolewa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo visiwani humo.

Huduma hiyo inayotolewa bila malipo katika kambi maalumu ya siku tano inafanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo, Januari 24, 2023 Visiwani Zanzibar wananchi waliofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo walisema kupatikana kwa huduma hiyo imewapa unafuu wa kutokufata huduma hiyo Dar es Salaam.

Saada Simba mkazi wa Fuoni, alisema baada ya kusikia wataalamu wa moyo watakuwepo katika hospitali hiyo alifika kwa ajili ya kupima afya yake ,amefarijika kwani amepata huduma nzuri na kwa wepesi.

“Mimi nina tatizo la shinikizo la juu la damu (BP), baada ya kufanyiwa vipimo leo nimekutwa sina tatizo lolote zaidi ya hili nililokuwa nalo, nashukuru sana nimepewa ushauri na nimeongezewa dawa nyingine ya kutumia ambayo ninaenda kuichukua dirishani bila malipo yoyote yale”, alisema Saada.

Naye Juma Amoor alisema  akiwa kazini mwaka 2019 alipata mshtuko wa moyo, kwani mapigo yake yalikuwa yanadunda kwa kasi alifanyiwa uchunguzi na kuandikiwa dawa za kutumia lakini alifika hapo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi na kujua tatizo ni nini.

“Nawashauri wananchi wenzangu tujenge tabia ya kupima afya zetu pindi tunaposikia wataalamu kama hawa wamefika katika maeneo yetu twendeni kupima. Baada ya kufika hapa leo nimepima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO), mfumo wa umeme wa moyo (ECG), kiwango cha sukari mwilini, shinikizo la damu, urefu na uzito bila malipo yoyote yale”, alisema Amoor.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha utafiti na mafunzo cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Pedro Pallangyo, alisema taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kusogeza huduma zake kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo na kuwapatia huduma ya upimaji na matibabu ya moyo.

Alifafanua na kusema kuwepo kwa huduma hiyo kumewasaidia wananchi kupata huduma ya ushauri wa lishe na matumizi sahihi ya dawa, vipimo na matibabu ya moyo kwa wakati tofauti na ambavyo wangesafiri na kuifuata huduma hiyo Dar es Salaam, pia wanaokutwa na matatizo wanapewa rufaa ya kwenda kufanyiwa uchunguzi zaidi katika taasisi hiyo.

“Ninatoa wito kwa wananchi kufuata mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kupunguza matumizi makubwa ya sukari, chumvi na vyakula vyenye mafuta, kupunguza unywaji wa pombe na kuacha kutumia bidhaa aina ya tumbaku kwa kufanya hivyo wataepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo,” DktPedro alisema.

Katika kutoa huduma ya kuwafuata wananchi mahali walipo Taasisi hiyo kwa mwaka 2022 ilifanya upimaji na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Geita, Mtwara na Lindi na kuwahudumia watu 3,935.

Aidha kati ya watu 3,935 waliohudumiwa, 1,391 walikutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la damu, kutanuka kwa misuli ya moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, matundu ya moyo hasa kwa watoto na valvu za moyo zilizoharibika na wagonjwa 335 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button