Habari

Wasaidizi kazi za ndani wapewa mafunzo

WAAJIRI wa wasaidizi wa kazi za ndani wameshauriwa kuishi vizuri na wasaidizi wao kwa kuwasikiliza na kuwarekebisha kwa upendo wanapokosea,  kwani wana nafasi kubwa katika malezi na makuzi ya watoto.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam  na Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni,  wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya wasaidizi wa kazi za ndani zaidi ya 100.

Dk Nyoni amesema awali walilenga kufikia wasichana 50, lakini maombi yaliyowafikia ni zaidi ya 200 hivyo watafanya mafunzo hayo zaidi siku zijazo.

“Leo tuna program ya kuwajengea uwezo wadada wa kazi katika malezi na makuzi ya mtoto, tumeifanya  hili tukiwa tunaelekea kuadhimisha siku ya ustawi wa Jamii  Machi 21,” amesema.

Dk Nyoni ameeleza kuwa hivi karibuni kumekuwa na kelele nyingi na malalamiko kuhusu malezi na tabia za watoto, kwa hiyo wakaona kama mchango wao wawe na vipindi na wasaidizi hao ambao wanalea watoto nyumbani kwa sababu wanakaa na watoto muda mrefu.

Amesema akina mama wengi wanaondoka asubuhi na kurudi jioni na  mtoto anakaa na dada, lakini dada hana uelewa kuhusu malezi na makuzi na ana mchango mkubwa katika kulea.

“Lakini tunatambua dada huyu kuna siku atakuwa mama ni muhimu kuelewa ni namna gani anapaswa kulea mtoto kutokana na mabadiliko tunamjenge uwezo wa kumuelewa mtoto na kuwa na msaada chanya katika maendeleo na makuzi ya mtoto,”amesisitiza.

Amebainisha kuwa baada ya kutoa tangazo hilo watu wanaokaa na wadada wa kazi wengi walisema wanakuja kuwahamasisha kupata haki zao, ambapo dhana hiyo inamaanisha kuwa hawakai nao vizuri.

“Niwasihi sana hawa ni wale ambao tunawaachia watoto tukae nao vizuri, hakuna binaadamu ambaye hana mapungufu, aelekezwe vizuri kwa sababu ndio tunawaachia watoto jinsi unavyokaa naye vibaya anaweza kuhamishia kwa watoto wana nafasi kubwa sana katika malezi na makuzi ya watoto,”ameeleza.

Ameeleza kuwa wakati mwingine ukatili unatokea kwa sababu dada hamuelewi mtoto kama dada atamuelewa na atajua namna ya kumsaidia  na mama pia anatakiwa kumsaidia dada awe katika mazingira ya kujiamini anavyomlea mtoto .

 

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button