
JESHI la Polisi mkoani Geita limewakamata watoto 20 kwa tuhuma za kuzurura mtaani usiku na kujihusisha na vitendo vya unyang’anyi, udokozi na uporaji mjini Geita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Safia Jongo ametoa taarifa hiyo Februari 8, 2023 mbele ya waandishi wa habari na kueleza hayo ni mafanikio ya operesheni maalum iliyofanyika.
Amesema watoto wote waliokamatwa wana umri chini ya miaka 15 na walikutwa wakizurura hovyo saa nane za usiku na baada ya kufanyiwa mahojiano wamebainika kujihusisha na uporaji.
“Lakini wengine ni wadokozi wa mifukoni , wanapora watu baada ya kulewa.
“Nia ni moja, kwanza kupunguza uharifu ambao unachangiwa na watoto hawa, lakini pili ni kumlinda mtoto kwa sababu idadi kubwa ya watoto hawa wapo chini ya miaka 15.
“Tutafanya ufuatiliaji kujua wazazi wao, kwa nini watoto hawa wapo mtaani, kama wametoroka wazazi ni hatua gani wamezichukua kuhakikisha kwamba hawa watoto wanapata matunzo,” amesema.