Habari

Watu 8 kati ya 100 wana vimelea vya Malaria Katavi

Imeelezwa kuwa watu 8 kati ya 100 mkoani Katavi wana vimelea vya Malaria. Utafiti uliofanywa mwaka 2022 kwenye ngazi ya jamii umebainisha.

Takwimu hizo zimetolewa leo na Dk. Dustan Bishanga kutoka taasisi ya afya ya Ifakara ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa ‘SHINDA MALARIA’ katika uzinduzi wa kampeni ya mradi huo unaotekelezwa katika Halmashauri za Tanganyika na Nsimbo.

Wakati Dk. Bishanga akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, mradi unaotekelezwa na Taasisi hiyo kwa ufadhili wa USAID|PMI amesema, Mkoa wa Katavi ni kati ya mikoa saba ambayo Wizara ya Afya imeitambua kama mikoa yenye maambukizi ya hali ya juu ya ugonjwa wa Malaria.

Amesema katika kuhakikisha mapambano dhidi ya Malaria yanafanyika afua mbalimbali zinafanyika katika vituo vya Afya na ngazi ya jamii kwa kutoa huduma ya mkoba katika maeneo ambayo ni ngumu kufikika kwa kushirikiana na timu za uendeshaji na usimamizi wa afya za Mkoa na Halmashauri husika.

Amesema katika kipindi cha miezi 7 mradi umetoa mafunzo kwa watoa huduma 36 watakaoweza kutoa huduma za Malaria ngazi ya jamii na watoa huduma waelimishaji 58 ikiwemo kuwapatia vitendea kazi.

“Umuhimu wa huduma hizi umejidhihirisha kwamba kati ya watu waliohudhuria hapa leo wameshapimwa mpaka sasa huduma zinaendelea watu takribani 100 na kati ya hao watu 3 kati ya watu 10 wamekutwa na vimelea vya Malaria, watu 3 kati ya 10 ni wengi sana katika takwimu za kawaida”

Mwakilishi wa USAID|PMI Lulu Msangi amesema toka mwaka 2020 PMI kwa kushirikiana na Serikali imesaidia uimarishaji wa ubora wa vituo vya afya katika kutoa huduma bora za afya ambapo juhudi hizo zimepunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini kutoka asilimia 18 mwaka 2015 mpaka asilimia 8 mwaka 2020.

Aidha, ili kuendelea kupunguza ugonjwa wa Malaria mkoani Katavi PMI imetoa msaada wa vitendelea kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambavyo ni Baiskeli 21, Mikoba ya kuwekea vifaa 21, vipima joto 21, mizani ya kupimia uzito ya mgonjwa 21, masanduku 21 yaliyo na vifaa vya afya zikiwemo simu za mkononi 36 kwa ajili ya watendaji wa afya ngazi ya jamii na simu 26 za ziada vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 47.5

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ametoa wito kwa watoa huduma za afya kuwa waadilifu katika kuwahudumia wananchi na atakaye bainika kwenda kinyume ikiwemo kutumia lugha mbaya pamoja na kutumia vibaya vifaa vilivyokabidhiwa atachukuliwa hatua za kisheria.

Pia amewataka wananchi kuacha imani potofu hasa kwa magonjwa ya mripuko ikiwemo Surua na kipindupindu badala yake wafike kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu ikiwemo chanjo mbalimbali za maradhi mengine.

Mrindoko amewaomba wafadhili wa mradi wa ‘SHINDA MALARIA’ kupanua wigo ili huduma hiyo iweze kutolewa katika Halmashauri zote tano za Mkoa huo.

Mradi huo unaofadhiliwa na USAID|PMI na kutekelezwa na Taasisi ya afya ya Ifakara ulianza kutekelezwa agosti 2022 na unatekelezwa kwa ufanisi katika Mkoa wa Katavi pekee Tanzania nzima kwa muda wa miaka mitano katika Halmashauri hizo mbili.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button