Habari

Wavunjifu wa sheria barabarani kufutiwa leseni

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Asas amelitaka jeshi la Polisi kukitumia bila woga kifungu cha 27 na 28 cha sheria ya usalama barabarani kuwafungia au kuwafutia leseni madereva watakaotenda makosa yanayohitaji adhabu hizo.

Ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa stika za usalama barabarani na ukaguzi wa hiyari wa vyombo vya moto uliofanyika stendi kuu ya zamani mjini Iringa leo.

“Utii wa sheria za barabarani ni changamoto kubwa sana, madereva wengi wa vyombo vikubwa vya moto ni kama wameshazoea kulipa faini kwa makosa wanayofanya na wakati mwingine wanatumia rushwa kujinasua kwenye makosa hayo. Matokeo yake bado tuna ajali nyingi barabarani zinazohatarisha uhai na usalama wa watu na vyombo hivyo,” alisema.

Aliyataja maeneo mawili ambayo ni hatarishi kwa ajali mkoani Iringa kuwa ni pamoja na Mlima Kitonga kwa upande wa barabara ya Iringa Dar es Salaam na Mlima Nyang’oro kwa upande wa barabara ya Iringa Dodoma,” alisema.

Kwa upande wa madereva wa bodaboda na bajaji, Asas alilitaka jeshi hilo kushirikiana na wadau mbalimbali wa usalama barabarani kuendelea kuwapa elimu akisema vituko wanavyofanya barabarani na kusababisha ajali vinatokana na uelewa mdoga wa sheria hizo.

“Ukiwaona wanavyoendesha vyombo hivyo barabarani unawezafikiri wako kwenye michezo ya kompyuta. Kuwanusuru wao na abiria wao ni muhimu tukaendelea kuwapa elimu,” alisema.

Awali Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa Wilaya ya Iringa, Glory Mtui alitoa elimu ya usalama barabarani na kuwataka madereva kujiepusha kuendesha vyombo vya moto wanavyotilia mashaka usalama wake au wakiwa wamelewa au wagonjwa.

Akisoma risala ya jeshi hilo, Kamanda wa Usalama Barabarani wa Wilaya ya Kilolo, James Makweta alizungumzia baadhi ya changamoto zinazokikabili kikosi cha usalama barabarani kuwa ni pamoja upungufu wa trafiki na vifaa vya kufanyia kazi zikiwemo pikipiki na magari kwa ajili ya doria.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi aliwahimiza wamiliki na madereva wote wa vyombo vya moto kuhakikisha vyombo vyao vinakaguliwa ili viruhusiwe kuendelea kutumika barabarani.

Akizindua shughuli hiyo Mkuu wa Wilaya ya Iringa Verronica Kessy alisema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kuongeza usalama kwa watumiaji wake.

“Kazi ya kuboresha miundombinu ya barabara ni ya kudumu, wakati serikali ikiendelea kutekeleza jukumu hilo watumiaji wa barabara hakikisheni mnakabiliana ipasavyo na viashiria vinavyoweza kusababisha ajali,” alisema.

Akitoa mfano alisema katika baadhi ya maeneo imeshuhudiwa watoto wakipakiwa mbele ya dereva wa bodaboda jambo ambalo ni la hatari kwa afya ya mtoto kutokana na upepo na endapo chombo hicho kitafungwa breki ghafla.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button